Serikali imetoa jumla ya tani 372.4 za chakula kwa wilaya ya Bagamoyo ili kuweza kukabiliana na tatizo la njaa!!

Waziri wa Kilimo na Chakula Steven Wassira
Na Anna Nkinda – Maelezo, Bagamoyo
05/10/2009 Serikali imetoa jumla ya tani 372.4 za chakula kwa wilaya ya Bagamoyo ili kuweza kukabiliana na tatizo la njaa linaloikabili wilaya hiyo.
Hayo yamesemwa jana na Mkuu wa wilaya hiyo Magessa Mulongo wakati akieleza hali ya chakula kwa mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja katika wilaya hiyo .
Mulongo alifafanua kuwa tani 186.2 ziligawiwa bure kwa wananchi na tani 186.2 zilitolewa kwa utaratibu wa kuuza ambapo kilo moja iliuzwa Tshs.50.
“Vijiji 64 kutoka katika kata 16 zenye jumla ya watu 132,703 wameombewa msaada wa chakula kupitia TASAF kwa mradi wake wa uhakika wa chakula (FOOD Security)”, alisema.
Alizitaja sababu za wilaya hiyo kukabiliwa na njaa kuwa ni kutokana na mavuno hafifu msimu wa kilimo 2008/2009 kwani wilaya hiyo ina upungufu wa chakula cha mizizi na nafaka tani 39,270 na mikunde tani 6,356.
Eneo lenye upungufu mkubwa wa chakula linajumuisha kata za Msata, Mbwewe, Kibindu, Miono, Mkange, Lugoba, Ubena, Chalinze na Tawalanda ambako kuna waathirika 112,144 na eneo lenye upungufu wa kati wa chakula linajumuisha kata za Vigwaza na Kiwangwa zenye waathirika 14,846.
Mkuu huyo wa wilaya aliendelea kutaja eneo lenye upungufu kidogo wa chakula ambalo linajumuisha kata za Dunda, Magomeni, Yombo, Kiromo na Zinga zenye waathirika 15,550 na kufanya jumla ya waathirika wote kuwa ni 142,540 sawa na asilimia 53 ya wakazi wote.
Kwa upande wake Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) aliwataka wakazi wa wilaya hiyo kutunza chakula walichonacho na kutokiharibu wakati wa sherehe za kuwacheza ngoma watoto wao.
“Siwakatazi kucheza ngoma, ngoma chezeni lakini muwe na matumizi mazuri ya chakula kwani mkiangalia hali halisi hivi sasa wilaya hii inkabiliwa na njaa hivyo basi kuna haja ya kutunza chakula kilichopo”, alisema Mama Kikwete.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment