MKUTANO MKUU WA SEKTA YA MAENDELEO YA JAMII KUFANYIKA MOROGORO!!

Mariam J. Mwafisi Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, itaendesha Mkutano Mkuu wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii wa Mwaka 2009 kuanzia tarehe 23 – 25 Septemba, 2009 mjini Morogoro. Wajumbe wa Mkutano huu ni watumishi kutoka Wizarani, Vyuo vya Maendeleo ya Jamii, Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi, Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Mikoa, Maafisa Maendeleo ya Jamii (DCDO) katika Halmashauri zote za majiji, manispaa, miji na wilaya na wageni waalikwa kutoka sekta nyingine. Aidha, kutakuwa na wawakilishi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira; Ofisi ya Waziri Mkuu -Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Uratibu wa Sekta, Wizara za Maji na Umwagiliaji; Kilimo, Chakula na Ushirika; Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii; Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi; Wizara ya Mambo ya Ndani; Wizara ya Kazi, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto - Zanzibar na wawakilishi kutoka katika Mashirika Yasiyo ya Kiserikali TACAIDS.

Madhumuni ya Mkutano huo ni kujadili utendaji wa kazi za Sekta ya Maendeleo ya Jamii na kuweka malengo na mikakati ya kuboresha utekelezaji wa majukumu ya Sekta hii. Aidha, kupitia Mkutano huu Wajumbe wa Mkutano hupata fursa ya kubadilishana uzoefu wa shughuli mbalimbali za maendeleo zinazofanyika katika maeneo wanayotoka. Kauli mbiu ya Mkutano wa mwaka huu ni “KILIMO KWANZA: MSINGI WA MAENDELEO YA JAMII”. Kaulimbiu hii imebuniwa ili kuiwezesha sekta kujiwekea mikakati ya jinsi itakavyotoa mchango wake katika utekelezaji wa Azimio la Serikali la ‘Kilimo Kwanza.

Katika mpango wake wa mwaka 2009/10, Wizara imepanga kuvipatia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vilivyomo katika mikoa sita (6) iliyopewa kipaumbele katika utekelezaji wa Azimio la Kilimo Kwanza matrekta ya kusukuma kwa mikono ‘‘power tillers’’ na majembe ya kukokota na ng’ombe. Jumla ya vyuo vitakavyopatiwa ‘‘Power Tillers’’ ni 23 katika mikoa ya Kigoma, Iringa, Morogoro, Rukwa na Ruvuma. Halikadhalika, Wizara imepanga kusambaza teknolojia nyingine zitakazowawezesha wananchi, kupunguza mzigo wa kazi hususan wanawake, kuongeza ufanisi na tija kupitia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi.
Mariam J. Mwafisi

KATIBU MKUU

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment