BODI YA UKAGUZI WA FILAMU YAZINDULIWA LEO!!

Waziri wa habari Utamaduni na Michezo George Mkuchika.

Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
29/8/2009, Dar es salaam
Serikali imepiga marufuku maonyesho yote ya filamu kwenye hadhara ya watu, majumba yasiyo rasmi,vibanda ,kumbi ndogondogo, hoteli na maeneo ya baa bila kufuata masharti ya jumba la sinema na kwa mujibu wa sheria na 4 ya mwaka 1974 inayotumika nchini.


Agizo hilo limetolewa leo jijini Dar es salaam na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo George Mkuchika wakati wa Uzinduzi wa Bodi ya Ukaguzi wa Filamu nchini ambayo itakuwa na jukumu la kukagua na kusimamia maonyesho na shughuli za filamu nchini.


Amesema sehemu nyingi zinazotumiwa kuonyesha filamu hazina leseni halali za kuonyeshea filamu na kuongeza kuwa sio salama kwa mali na afya za watu.
“Nachukua fursa hii kutoa onyo kwa mtu yeyote atakayeonyesha filamu kwenye hadhara ya watu katika majumba yasiyo rasmi ,vibanda,kumbi ndogondogo,hotelini, baa na katika vyombo vya usafiri waache mara moja” amesisitiza.
Amefafanua kuwa sehemu nyingi zinazotumika kuonyeshea filamu sasa hazikidhi matakwa ya ujenzi wa kumbi za kuonyeshea filamu na ni kinyume cha sheria kwani nyingi zimekuwa chanzo cha maficho ya wahalifu, majambazi, biashara ya dawa za kulevya na kuchochea vitendo vya ngono kwa vijana.
Amesema athari nyingi tayari zimeshajitokeza katika jamii yetu na kuongeza kuwa filamu nyingi zimechangia kubomoa na kudunisha Utamaduni wa taifa letu na hata kuchangia kwa kiasi kikubwa kubomoa misingi ya amani , Upendo , Uadilifu,heshima, uaminifu na utu ambao ni utambulisho wa mtanzania jinsi ulivyokuwa umejijenga na kuenea katika jamii yetu.
Waziri Mkuchika amewataka wanaojishughulisha na shughuli za kuonyesha filamu kwa kuzingatia sheria na kufuata kanuni za nchi licha ya kuwa ya fani ya filamu kukuza ni biashara na inakuza uchumi na pia kuleta maendeleo na kuwataka kuepuka kuonyesha filamu zinachochea vitendo viovu na mmomonyoko wa maadili ndani ya jamii kutokana na filamu nyingi kutokaguliwa na kupangwa katika madaraja kulingana na matakwa ya watanzania.
Awali akizungumza kuhusu majukumu ya Bodi hiyo amesema kuwa Bodi itakuwa na jukumu la kuweka misingi ya kuimarisha utaratibu wa usimamizi wa utengenezaji wa filamu na pia kutoa vibali vya kutengeneza filamu hapa nchini.
Mbali na jukumu hilo Bodi ya Ukaguzi wa Filamu itakuwa na jukumu la kuratibu, kusimamia na kushauri namna ya kukuza Tasnia ya Filamu kwa kuzingatia sera ,sheria na kanuni zikiwemo taratibu na miongozo mbalimbali ya nchi hasa sera ya Utamaduni na Sheria ya Filamu na Michezo ya kuigiza.
Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo Bi. Rose Sayore ameihakikishia serikali kuwa Bodi yake itafanya kazi kwa mujibu wa sheria na kuhakikisha kuwa kanuni, sheria , maadili na taratibu za uonyeshaji na utengenezaji wa filamu zinazingatiwa kwa maslahi ya watanzania na vizazi vijavyo.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment