WAMA YACHANGIA MILIONI NNE KWA SACCOS MBILI MKOANI IRINGA!!

Mke wa Rais mama Salma Kikwete akisalimia wananchi katika moja ya mikutano aliyowahi kuifanya kwa shughuli mbalimbali za kijamii.

Na Anna Nkinda – Maelezo
02/02/2009 Iringa Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (MAWA ) kupitia Taasisi yake amechangia shilingi milioni nne kwa vyama viwili vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCOS) vya Wanawake wa wilaya za Iringa na Kilolo na wanawake wa Iringa mjini mbazo zitawasaidia kuinua mtaji na kununua vitendea kazi kwa ajili ya SACCOS hizo.
Mama Salma alitoa mchango huo jana (leo) alipokuwa akiongea na wanawake hao kwa nyakati tofauti wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani humo.
“Mwanamke akiwa na uchumi wa kutosha unaweza kumsaidia kutatua matatizo yake pasipo kutegemea msaada kutoka upande mwingine na hivyo kuwa mwanamke imara katika jamii”, alisema mama Kikwete.
Aliendelea kusema kuwa kila anayekopa ahakikishe anatumia mkopo wake kwa matumizi yaliyokusudiwa na vilevile ahakikishe analipa deni lake kwa wakati. Kwani kwa kufanya hivyo SACCOS hiyo itaendelea kushamiri na wanachama wote wataendelea kunufaika lakini wachache wakianza ukorofi mtaji wa SACCOS utapungua na Saccos itayumba.
Akisoma taarifa ya SACCOS ya wanawake wa wilaya za Iringa na Kilolo mbele ya mgeni rasmi Mama Kikwete, ambaye alifungua mkutano mkuu wa mwaka wa SACCOS hiyo uliofanyika katika ukumbi wa chuo kikuu Huria kilichopo mjini Iringa,mtunza hazina wa SACCOS hiyo Salma Lupenza alisema kuwa mtazamo wao ni kuendelea kuwahamasisha wanawake wa vijijini na katika kata zote ili wajiunge na kunufaika na SACCOS hiyo.
Kwani kwa kufanya hivyo mtandao wa huduma za kifedha vijijini utawafikia wanawake walio wengi ambao ndio wazalishaji wakuu katika kaya na utunzaji wa familia.
Sehemu ya taarifa hiyo ilisema kuwa , “Hivi sasa wanaume katika kaya wamekuwa wakitoa uhuru kwa wake zao kujiunga na SACCOS kwa vile wamekuwa wakielimishwa mara kwa mara kuhusu masuala ya jinsia na wengine wamefikia uamuzi wa kujiunga na SACCOS yetu”.
Mtunza hazina huyo aliyataja matatizo yanayowakabili kuwa ni uchache wa vitendea kazi, uchache wa fedha za ndani ukilinganisha na mahitaji ya mikopo kwa vile wanachama ni wengi kuliko mtaji walionao, ukosefu wa elimu na mafunzo ya kutosha.
Kuhusiana na uchache wa fedha za ndani Lupenza anasema kuwa hivi sasa wanafanya maandalizi ya kupata mkopo toka mfuko wa Rais wa ujasiliamali hata hivyo wanawakaribisha awadau mbalimbali kuwaunga mkono kwa kuwasaidia mtaji au zana zitakazowezesha ufanisi katika uendeshaji wa chama.
SACCOS hiyo ilianza mwaka 2003 na kusajiliwa rasmi mwaka 2007 wakati huo ikiwa na wanachama 113 hivi sasa ina wanachama zaidi ya 500 ambao ni wanawake na wanaume.
Idadi kubwa ya wanachama wa SACCOS hiyo ni kutoka vijijini wengi wao wakiwa ni wajane ambao wameweza kuweka na kukopa na kujiajiri wenyewe kwa kuendesha biashara ndogondogo, kilimo, ufugaji na kuweza kusaidia familia kwa mahitaji yao muhimu kama chakula, malazi na elimu.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment