AU YAITAKA MOURITANIA KUITISHA UCHAGUZI WA KIDEMOKRASIA IFIKAPO MWEZI JUNI MWAKA HUU.

Rais Muammar Gaddafi wa Libya ambaye pia ni mwenyekiti wa AU
3/3/2009. Dar es salaam.
Umoja wa Afrika (AU) umemtaka kiongozi aliyefanya mapinduzi ya Kijeshi nchini Mouritania kuhakikisha kuwa anaitisha uchaguzi wa kidemokarasia nchini humo ifikapo mwezi june mwaka huu.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es salaam na Mwenyekiti wa Baraza la mawaziri wa Afrika (AU) Dkt. Ali Abdusalam Tourek wakati akiongea na waandishi wa habari.
Dkt Ali ambaye aliongozana na Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania Bernard Membe katika mkutano huo amesema kuwa jana alikutana na rais Kikwete akimletea salam za Rais wa Libya na mwenyekiti wa AU kanal Gadafi kuhusu maendeleo ya juhudi za kutatua migogoro inayoendelea barani Afrika.
Amesema kuwa katika mazungumzo yao walizungumzia migogoro barani Afrika akigusia mapinduzi yaliyofanyika Mouritania mwezi August mwaka jana na maamuzi yaliyofikiwa na Umoja Afrika.
Kuhusu kiongozi wa jeshi aliyefanya mapinduzi mwezi August mwaka jana amesema kuwa ataachia madaraka yake kwa spika wa bunge la nchi hiyo mwezi ujao ili na yeye aingie katika mchakato wa kugombea nafasi ya urais wa nchi hiyo utakaowajumuisha viongozi waliokuwepo madarakani na wale waliopinduliwa kuingia katika kinyanganyiro cha urais kufutana na matakwa ya AU katika uchaguzi wa Kidemokrasia utakaofanyika mwezi June mwaka huu.

“Tunatarajia kuwa mwishoni mwa mwezi wa sita mwaka huu nchini Mouritania kutakuwa na serikali halali iliyochaguliwa na wananchi” Amesema.
Ameongeza kuwa uchaguzi utakapokamilika viongozi mbalimbali wa nchi za Afrika watajumuika pamoja kushuhudia kuapishwa kwa rais mpya wa nchi hiyo na kwa hatua hiyo nchi ya Mouritania itakuwa imeruhusiwa kuingia kwenye Umoja wa Nchi za Afrika.
Kuhusu machafuko yanayoendelea nchini Sudani eneo Darfur Dkt. Treaky amesema kuwa suala la mahakama ya kimataifa kumtaka rais Omari Bashiri wa Sudan ashitakiwe katika baraza la usalama la umoja wa mataifa haliungwi mkono na Rais Gadafi ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa AU kutokana na kuwa kikwazo cha mchakato wa amani nchini humo.
“Kumkamata rais Bashiri kutaathiri sana juhudi na oparesheni za kutafuta amani nchini humo jambo ambalo hatuliungi mkono” Amesisitiza.
Ameongeza kuwa msimamo wa Kanali Gadafi ni msimamo wa Libya, Afrika na nchi za Kiarabu , kwamba mchakato wa kumkamata rais Bashir asingependa uendelee kutokana na kutakuwa kumezorotesha kwa kiasi kikubwa maendeleo na mchakato uliopo kuelekea amani nchi Sudan.
“ Kumkamata rais Bashir kutakuwa kumekwamisha juhudi za Amani kutokana na uwezekano wa nchi ya Sudan kuzuia majeshi ya Umoja wa Afrika yasipelekwe ili kulinda amani wakati mchakato wa utafutaji wa amani ya kudumu kuendelea”
Kuhusu uchumi amesema kuwa Libya itaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania na nchi nyingine za Afrika katika kuwekeza katika sekta ya kilimo kwa kuhakikisha kuwa juhudi mbalimbali za kuinua sekta ya kilimo zinafanikiwa ikiwemo ya kuanzishwa kwa Benki ya Kilimo itakayowasaidia wakulima kwa kuwakopesha waweze kupata mbegu bora za kilimo, kutoa mikopo kwa wakulima pamoja na kuwa na kilimo cha umwagiliaji na madawa ili kuhakikisha kuwa wakulima hapa nchini wanafaidika kutoakana na shughuli za kilimo.
Amesema kuwa ili kufanikisha suala hilo hususani mapinduzi katika sekta ya kilimo mawaziri wa nchi hizi wanaoshughulikia sekta ya kilimo ili kuwa mchakato wa pamoja wa namna ya nchi hizi kuanza kushirikiana katika sekta ya kilimo.
Waziri huyo baada ya kuondoka Tanzania ataelekea nchini Comoro na pia Djibout na baadaye kuonana Mwenyekiti wa AU ili kutoa taarifa ya ziara yake.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment