MWALIMU HAFSA LUMBU AKIWAFUNDISHA WANAFUNZI WAKE!!

Mwalimu Hafsa Lumbu akiwa na wanafunzi wake

Kufundisha na kuwa mwalimu ni vitu viwili tofauti unaweza kuwa mwalimu nausiweze kufundisha wala usiwe na wito wa kufundisha na unaweza usiwe mwalimu kwa maana kupata mafunzo ya ualimu lakini ukawa na uwezo wa kuelekeza jambo mpaka mwanafunzi wako au unayemuelekeza akakuelewa vizuri kuliko hata mtu ambaye amepitia mafunzo ya ualimu.

Sisemi kuwa haina maana kwa mtu yeyote anayetaka kuwa mwalimu kwenda shuleni kupata mafunzo na mbinu mbalimbali za kujua namna ya kufundisha la hasha nina maana hata kama utakwenda shuleni kupata hayo mafunzo ya namna ya kufundisha wanafunzi lakini pia ni muhimu muhusika akapenda kile anachotaka kukifanya na akawa na wito nacho,uvumilivu na kujiamini.
Haya ndiyo mambo yanayoweza kumfanya mwalimu aweze kufanya kazi yake kwa ufanisi zaidi na kuwafanya wanafunzi wake wamuelewe vizuri wakati anapowafundisha darasani, kuna watu ambao wanazaliwa na kukua wakiwa ni walimu kabla hata hawajapata hayo mafunzo ya ualimu watu kama hawa wanapopata nafasi ya kusomea kazi ya ualimu wanaweza kuwa walimu wazuri sana kwa kuwa tayari wanaipenda kazi ya kufundisha.
Kama vile mtoto huyu Hafsa Lumbu niliyemkuta mataani kwao maeneo ya Temeke Mtoni kwa Azizi Ally akiwa amewakusanya watoto wenzie akiwafundisha Hisabati,ilinibidi nikatishe safari yangu nikasimama na kumwangalia kwa muda mrefu jinsi alivyokuwa akiwaelekeza wanafunzi wake jinsi ya kukokotoa hisabati kweli alionyesha uwezo mkubwa na wanafunzi wake walikuwa wametulia kimya wakiandika na kufuata maelekezo aliyokwa akiwapa, ilinivutia kwakweli nikaamua kuchomoa Camera ya FULLSHANGWE na kumpiga picha.

Baada yakumpiga ile picha nikamuuliza jina lake akaniambia anaitwa Hafsa Lumbu, nikamuuliza tena wewe unapenda kwa mwalimu?akanijibu "ndiyo napenda sana kuwa mwalimu ndiyo maana nimeamua kuwafundisha hesabu wadogo zangu badala ya kwenda kucheza mdako" haya yalikuwa ni majibu yenye faraja sana kwangu mtoto huyu anahitaji kuungwa mkono na kila mtu hasa wazazi wake ambao ndiyo wako naye wakati wote nawaomba wampe muda wa kutosha kujisomea na kujifanyia mazoezi ya masomo yake kila wakati.
Mimi wakati nasoma shuleni kwetu wakati huo tuliwahi kuwa na mwalimu mmoja sitapenda kumtaja jina wa shule yenyewe, ambaye darasa lake lilikuwa linaongoza kufeli kila somo alilokuwa akipangiwa kulifundisha kwa wakati huo ilikuwa lazima wanafunzi nusu ya darasa wafeli
Ukafanyika uchunguzi kwamba kwa nini kila anapopangiwa darasa fulani mwalimu huyo lazima wanafunzi wafeli?, ikagundulika kuwa kwanza yeye mwenyewe alikuwa hapendi kazi ile ya kufundisha, pengine pia hakuwa na wito kwa kazi ya ualimu lakini pia wanafunzi walikuwa wakimwogopa sana kwani ilikuwa kila anapofundisha silaha yake kubwa ili mwanafunzi amwelewe ni kuzungumza kwa ukali na viboko , kwa hiyo alikuwa anaweza kuja darasani akawa mkali sana mfano akamuuliza mwanafunzi mmoja swali mwanafunzi yule akikosa kujibu tu mtacharazwa viboko darasa zima, hivyo wanafunzi walijenga hofu zaidi kwa mwalimu huyo, akiingia tu darasani wanafunzi wote wanakuwa tayari wameshachanganyikiwa kwakuwa wanajua kuingia kwa mwalimu wao huyo darasani tayari ni hali ya hatari kwao.
Mwalimu huyu angekwa na wito kama mtoto huyu pengine asingefanya aliyokuwa akiyafanya wakati huo maana angekuwa anaipenda kazi yake na angekuwa anajiamini na mwenye ujasiri wa kufundisha watoto hiyvo wangemwelewa vizuri na wasingemwogopa, ila wangemfanya kuwa mwalimurafiki na wala wasingeogopa kujibu wala kuuliza maswali FULLSHANGWE inamtakia kila mafanikio mtoto Hafsa Lumbu ili aje kuwa mwalimu mzuri wa baadae katika nchi yetu nzuri Tanzania.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment