Zain yaleta show ya sarakasi kabambe Dar!!


Wasanii wanaounda kundi la sarakasi la Zain Sarakasi Mama Afrika lenye wasanii 65, wakionyesha umahiri wao wakati wa utambulisho kwa waandishi wa habari, Dar es Salaam jana. Shoo hiyo ya sarakasi itazinduliwa rasmi nchini Novemba 26, mwaka huu


Meneja Masoko wa Zain Tanzania, Costantine Magavilla akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana wakati wa utambulisho wa kundi la sarakasi la Zain Sarakasi
Mama Afrika, litakaloanza kufanya maonyesho yake nchini Novemba 26, mwaka huu Masaki, Dar es Salaam. Katikati ni Mkurugenzi na muandaaji wa shoo hiyo, Winston Ruddle kutoka Zimbabwe na kulia ni Ofisa Uhusiano wa Zain Tanzania, Celine Njuju.



Shoo kabambe ya sarakasi ya kwanza ya aina yake barani Afrika itakayojulikana kama Zain Mama Afrika Circus itaanza kuonyeshwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam. Shoo hiyo ya sarakasi ya kusisimua itakuwa ya saa mbili na nusu na itakuwa inaonyeshwa Masaki, Dar es Salaam.

Mkurugenzi na muandaaji wa shoo hiyo, Winston Ruddle kutoka Zimbabwe, amesema sarakasi hiyo ya aina yake imedhaminiwa na kampuni ya simu ya mkononi ya Zain Tanzania na itakuwa na wasanii wenye vipaji wapatao 65 kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika ikiwemo Tanzania na itazinduliwa rasmi Novemba 26, mwezi huu.

“Ni shoo ya sarakasi ya aina yake. Tumejiandaa kwa kipindi cha miaka sita na tutawasisimua watazamaji wa rika zote kuanzia watoto hadi watu wazima. Tutakuwa na maonyesho yenye utajiri wa utamaduni wa Afrika,” alisema Ruddle.

Wasanii wote ni Waafrika. “Watazamaji watajionea wasanii wakifanya maonyesho ya aina yake na watapata thamani ya pesa zao,” alisema.

Hema kubwa la hadhi ya kimataifa lenye uwezo wa kubeba zaidi ya watu 1,000 limewekwa Masaki. “Itakuwa shoo ya kusisimua kuliko zote kufanyika nchini Tanzania. Wasanii, wanasarakasi na vionjo mbalimbali vitakonga nyoyo za watazamaji. Itakuwa ni shoo ya kukumbukwa. Wasanii wote wana vipaji vya kuzaliwa na wamepata mafunzo ya kina nchini Tanzania na nchi za nje. Wasanii watakaotumbuiza wanatoka Tanzania, Afrika Kusini, Zimbabwe, Kenya na Ethiopia na wana hadhi ya kimataifa,” alisema.

“Zaidi ya mavazi 500 ya kitamaduni yameandaliwa, vikaragosi na vionjo mbalimbali,” alisema Ruddle.

Meneja Masoko wa Zain Tanzania, Costantine Magavilla amesema Zain inaona fahari kusaidia kuleta shoo hiyo nchini Tanzania. “Tunayo furaha kushirikiana na waandaaji wa shoo hii ya sarakasi ya aina yake ambayo itaanza kuonyeshwa hapa Tanzania mwezi huu. Tunaamini Watanzania watasisimka na kufurahia shoo hii,” alisema.


Kutakuwa na maonyesho mawili kila mwisho wa wiki Jumamosi na Jumapili na onyesho lingine siku ya wiki ili kuwapa watazamaji muda wa kutosha wa kujionea sarakasi hiyo. Tiketi zitauzwa papo hapo Masaki kwa bei ya Tsh. 20,000, Tsh. 16,000 na Tsh. 8,000.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment