Na. Jamal Zuberi ,
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imewataka Wakurugeni wa Wilaya nchini kuhakikisha kuwa Maafisa watendaji wa Kata na Vijiji wanaapishwa kuwa walinzi wa amani kabla ya kutekeleza majukumu ya ulinzi wa amani.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti waTume hiyo Mhe.Amiri Ramadhani Manento wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mafunzo kwa watendaji wa serikali za mitaa katika mikoa ya Manyara, Mara, Mtwara, Shinyanga na Tanga kuanzia Februari 2010 hadi Machi 2010, mwishoni mwa wiki kwenye ukumbi wa Tume hiyo Dar es salaam.
Alisema kuwa katika vijiji vyote vilivyotembelewa katika kipindi hicho baadhi ya Maafisa watendaji wa vijiji na watendaji wa kata walikuwa hawajaapishwa .Alitoa mfano wa kata zote zilizotembelewa katika Wilaya za Newala na Nanyumbu kuwa watendaji hayo hawajaapishwa. Alisema kuwa zaidi ya watendaji wa serikali za mitaa 1000 walipatiwa mafunzo kuhusu utawala bora na uongozi bora na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini katika kipindi hicho.
Alisema kuwa kwa kipindi hicho tume ilitoa mafunzo na elimu kwa watendaji na viongozi wa seriklai za mitaa,ngazi ya tarafa, kata, mitaa, vijiji na vitongoji . ‘ tume imefanya mafunzo hayo kutokana na malalamiko mengi yanayopokelewa na Tume yanahusu watendaji katika ngazi za serikali kuu na serikali za mitaa’ aliongoza Manento.
Alisema kuwa tangu tume kuanzishwa mwaka 2001 imepokea jumla ya malalamiko 25,753 kutoka wananchi ambapo kati ya hayo 24,488 yalihusu ukiukwaji wa misingi ya utawala bora na 1,265 uvunjwaji wa haki za binadamu. Mkoa wa Dar es salaam na Mwanza inaongoza kwa malalamiko ya ukiukwaji wa utawala bora na haki za binadamu.
0 comments:
Post a Comment