PINDA – ASEMA MICHANGO YA CCM NI HIARI.


NA MAGRETH KINABO NA BENJAMIN SAWE, MAELEZO


DODOMA.


WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema kwamba michango ya kuchangia Chama cha Mapinduzi(CCM) kutoka kwa watu mbalimbali ni vizuri ikaendelea kuwa ni ya hiari na isiwe ya lazima.


Hayo yalisemwa na Waziri Mkuu Pinda jana Bungeni,wakati akijibu maswali ya papo kwa hapo kuhusu swali la Mbunge wa Karatu Dk. Willbroad Slaa( CHADEMA) lililouliza kuwa kuna taarifa mbalimbali na wana nyaraka za wakuu wa wilaya ambao wanatumia muda na vyombo vya Serikali kuwaita wafanyabisha bila ya kuwaambia wanaitiwa nini, wakifika kwao wanaambiwa wachangie CCM kati ya Sh,10,000 na 20,000.


Je Serikali inatoa tamko gani? Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu Pinda alisema Mkuu wa Wilaya ni Kamisaa wa CCM anawajibu wa kusaidia kutafuta michango kama kiongozi wa CCM tatizo ni endapo atatumia nguvu za dola kumshurutisha mtu kuchangia.


“ Ni tatizo kumshurutisha mtu kuchanga kama ni hiari halina tatizo hata sisi wa ndani ya Serikali tunachangia. Ni vizuri michango hii ikaendelea kuwa ya hiari,” alisema Waziri Mkuu Pinda.


Aliongeza kuwa mtumishi wa Serikali anaruhusiwa kuwa na chama chochote.


Akijibu swali la nyongeza la Dk. Slaa lililouliza kuwa haitakiwi kutumia ofisi ya Serikali, Waziri Mkuu Pinda alimtaka, amkabidhi makaratasi ili Serikali iweze kutoa maelekezo kwa wakuu hao waweze kujiepusha na matumizi hayo.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment