Magereza kusimamia Uchaguzi mwaka huu.


Katika kuhakikisha kuwa uchaguzi Jeshi la Polisi hapa nchini linamudu kusimamia Vituo vya kupigia kura vinavyokadiriwa kufikia elfu 55, Jeshi hilo limeamua kuwashirikisha askari Magereza pamoja na mgambo ili kusaidia kusimamia ulinzi na usalama wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni nchini kote.


Hayo yalisemwa Wilayani Magu mkoani Mwanza na Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la Polisi Paul Chagonja wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nyamikoma katika ziara yake ya siku tano ya ukaguzi wa maeneo mbalimbali ya Polisi, uhamasishaji wa Mpango wa Polisi Jamii pamoja na kukagua maandalizi ya ulinzi na usalama kwa upande wa Polisi mkoa wa Mwanza wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu.


"Katika uchaguzi wa mwaka huu tunategemea kuwa na Vituo vya kupigia kura karibu ya elfu 55 nchini kote lakini askari Polisi nchi nzima hatuzidi hata elfu 33 hata tukiwagawanya kila askari kuanzia askari wa mwisho mpaka IGP kwa kuweka askari mmoja mmoja katika kila Kituo bado askari wetu hawawezi kutosha…."



"Ni sababu hiyo basi tumeona kuwa tuweke mkakati maalum wa kuwajumuisha askari wa Jeshi la Magereza pamoja na mgambo ili kuhakikisha kuwa kila Kituo cha kupigia kura kinapata ulinzi mzuri na hatimaye wananchi washiriki vizuri katika kupiga kura" alifafanua zaidi Kamishna Chagonja. (Habari na mtandao wa Wanabidii)

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment