Waganga wa jadi, Dewji kuingia `mkataba’ leo!!

Azim Dewji kulia akiwa amekaa na Naibu Waziri wa Nishati Adam Malima na Mbunge wa Sumve Richard Ndasa.

WAKATI homa ya pambano la kukata na shoka kati ya timu ya soka ya Tanzania `Taifa Stars’ na Brazil ikizidi kupanda miongoni mwa mashabiki, waganja wa kienyeji nao wameibuka na kudai watahakikisha Stars inashinda ili waweze kuchukua donge nono la fedha lililoahidiwa na mwanamichezo na mfanya biashara maarufu nchini, Azim Dewji.Dewji, katikati ya wiki hii alizitaka Simba na Yanga kuachana na na masuala ya ushirikina katika soka na kuzitaka kuelekeza nguvu katika maandalizi na mazoezi ya nguvu kama kweli zinataka kupata mafanikio.

Katika kuonyesha hana imani na masuala ya ushirikina, aliwataka waganga wathibitishe uwezo wao kwa kuifunga Brazil, huku akiahidi kutoa kitita cha sh milioni 10 kwa kila mmoja wao, hata kama idadi yao itafikia zaidi ya 100.Jana, mmoja wa watu wa `kamati za ufundi’ katika soka, Sadick Maulid `Dk. Kalimauganga’ aliibuka na kusema kwamba, wamedhalilishwa na Dewji na kusisitiza watathibitisha hawabahatishi katika kazi yao kwa kuifunga Brazil.

“Mbona ni kazi ndogo tu, sisi tumejikusanya na wengi wamechukizwa na dharau ya Azim kwamba sisi ni matapeli. Tunaijua kazi yetu na tutaionyesha kwa Brazil ingawa ndiyo timu inayoongoza kwa ubora duniani,” alisema Kalimauganga, mwanachama maarufu wa Simba kama ilivyo kwa Dewji aliyewahi kuifadhili klabu hiyo na kuifikisha fainali za CAF mwaka 1993.Aliongeza kwamba, wanataka kukutana na Dewji na kuingia naye mkataba ili `asiwaruke’ endapo watatimiza azma ya kuifunga Brazil.

Naye Dewji, alijibu mapigo kwa kusema kwamba, kama wanajiamini, wajitokeza leo (saa 5 asubuhi) katika makao makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ili waingie mkataba na kupiga picha za utambulisho ili iwe rahisi kwao kulipwa fedha zao kama wataiweza kazi ngumu ya kuifunga Brazil.“Nakwambia hawa jamaa ni wajanja wajanja tu, hakuna uchawi katika soka bwana… sasa ni hivi, waambie wajikusanye kesho (leo Jumapili) saa 5 pale TFF, mimi nitakuja tukubaliane, wakishinda nimeahidi kila mmoja nitampa sh milioni kumi, lakini tukifungwa, wajue kibarua chao kitaishia hapo kwa sababu kwa wiki nzima nitawaomba wakubali kutangazwa kupitia vyombo vya habari kwamba hawa ni matapeli katika soka na wanaorudisha nyuma maendeleo ya mchezo huu,” alisema Dewji.

Kalimauganga na wenzake wamekubali kuitikia wito wa Dewji, huku wakisema ni yeye atakayepoteza fedha zake kwa kuwa wana uhakika na wanachokifanya.Stars na Brazil zinatarajiwa kuumana kesho jioni Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa kirafiki wa kihistoria baina ya timu hizo zisizolingana hata chembe katika uzoefu na ubora wa soka. Kwa Brazil, hiyo itakuwa mechi ya mwisho ya kujipima nguvu kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia mwishoni mwa wiki ijayo huko Afrika Kusini.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment