RAIA WA OMAN ABAMBWA NA MADAWA YA KULEVYA TABORA!


Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi

Jeshi la Polisi mkoani Tabora, linawashikilia watu wawili akiwemo Raia mmoja wa Oman kwa tuhuma za kupatikana na madawa ya kulevya aina ya Heroin.

Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Kamishna Msaidizi Liberatus Barlow, amewataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni Mbaraka Hemedi(34) Raia wa Oman na Mohammed Sharifu(41) Mtanzania mwenye asili ya Kiarabu.

Amesema kuwa watuhumiwa hao wamekamatwa huko Wilayani Igunga mkoani Tabora baada ya Raia wema kuwatonya Polisi juu ya kuwepo kwa watuhumiwa hao kwenye gari aina ya Toyota Chesser lenye namba za usajili T. 676 ANM huku wakijigunga sindano zenye madawa hayo.Amesema baada ya Polisi kuwakamata walifanya upekuzi zaidi ndani ya gari hilo na kufanikiwa kupata kete 18 za madawa hayo aina ya heroin ambayo thamani yake bado kufahamika mara moja.

Hata hivyo, Kamanda Barlow amesema tayari Makachero wa Jeshi la Polisi wakiongozwa na Mkuu wa Upelelezi mkoani humo ACP David Ambwene Mwakiruma, wamejikita zaidi katika utafuta wa taarifa za muhimu ili kubaini chimbuko la mtandao mzima unaojihusisha na biashara hiyo ya madawa ya kulevya.

“Lakini tunafanya Uchunguzi zaidi kuweza kuwa na uhakika wa chanzo cha madawa haya kwa sababu kwa mkoa wetu ni mara ya kwanza kufanikisha kukamatwa kwa madawa haya ya aina ya Heroin”. Amesema Kamanda Barlow.

Kamanda Barlow ameongeza kwamba kukamatwa kwa madawa hayo kunaonyesha wazi kuwa mikoa ya katikati mwa nchi nayo kwa hivi sasa haiko salama na huwezi ukaitofautisha na maeneo ya mikoa mingine kama ya Pwani na maeneo yanayopakana na nchi jirani.

Amepongeza ushirikiano uliopo baina ya Polisi na Raia na kwamba watuhumiwa hao wasingeweza kukamatwa kama sio taarifa za uhakika zilizotolewa kwa wakati muafaka ma raia wema wanaojitolea kupiga vita vitendo vya kihalifu hapa nchini.Kamanda Barlow amesema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kupatikana na dawa za kulevya.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment