Waziri mkuu Somalia agoma kung'atuka!!


Waziri Mkuu wa Somalia Umar Abdirashid Sharmarke, amewaambia waandishi wa habari mjini Mogadishu kuwa katiba haimruhusu Rais Sharif kumfuta kazi na hivyo yeye bado anaongoza baraza la mawaziri kihalali.

Baada ya Rais Sharif kutangaza kumteua waziri mkuu mpya, huku Spika wa bunge naye akitangaza kujiuzulu, mkutano wa dharura uliitishwa Ikulu mjini Mogadishu kati ya Rais na waziri mkuu.

Ni katika mkutano huo ambapo Bw Sharmarke alimwambia wazi Rais huyo kuwa kamwe hatowasilisha barua ya kujiuzulu.

Kulingana na vifungu vya 44 na 51 katika katiba ya muda ya Somalia, waziri mkuu anaweza kuondolewa madarakani na bunge ikiwa litapiga kura ya kutokuwa na imani naye.
Ulipozuka mzozo ndani ya bunge mwishoni mwa juma, spika wa bunge aliyejiuzulu Sheikh Adan Madobe, alisema kuwa bunge lilipiga kura ya kutokuwa na imani na serikali ya waziri mkuu Sharmarke.

Hata hivyo, waziri mkuu kasema hakuna kura iliyopigwa, jambo ambalo linathibitishwa pia na baadhi ya wabunge waliohudhuria kikao hicho.
Hali hii sasa inaiweka njia panda serikali ya Sheikh Sharif, ambayo hadi iingie madarakani miezi 18 iliyopita haikuweza kuleta maridhiano, wala kurejesha amani kulingana na ahadi ya rais Sharif wakati akila kiapo cha kuwa kiongozi wa nchi.

Mzozo huo ndani ya serikali umeibuka huku wapiganaji wa kiislam wakijaribu kuiangusha serikali ya mpito, ambayo hadi sasa inatawala kilo mita chache katika mji mkuu Mogadishu, ikisaidiwa na jeshi la Muungano wa Afrika.

Serikali ya mpito ikishindwa kumaliza tofauti zake na kusambaratika, uamuzi wa mwisho utakuwa juu ya jamii za kimataifa.
Kama jamii hizo zikiamua kukaa kimya itawapa wapiganaji nafasi nzuri ya kuiteka nchi nzima.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment