RASILIMALI ZA MISITU KATIKA KUCHANGIA PATO LA TAIFA.


Na Veronica Kazimoto – MAELEZO Dar es Salaam

Rasilimali za misitu zinakadiriwa kuchangia asilimia 2 hadi 3 kwenye pato la Taifa na zina umuhimu mkubwa sana hapa nchini kwa kuwa ni chanzo muhimu cha nishati inayotumika katika makazi yetu.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Maliasili na Utalii Shamsa Mwangunga wakati akizindua kamati ya kitaifa ya ushauri ya misitu iliyofanyika jijini Dar es Salaam ambapo amesisitiza kuwa misitu ni chanzo muhimu cha nishati, kwani asilimia 95 ya nishati hiyo hutokana na miti.

”Shughuli mbalimbali zinazofanywa katika maeneo mbalimbali ya misitu huchangia katika kuondoa umaskini miongoni mwa jamii ya Watanzania, iwapo haya yote yangeingizwa katika mahesabu ya pato la taifa mchango wa sekta ndogo ya misitu ungekuwa mkubwa kuliko kiwango kilichoainishwa hapo juu” Amesisitiza waziri Mwangunga.

Waziri Mwangunga amezindua kamati ya kitaifa ya ushauri ya misitu ambayo inaundwa na wajumbe 15 kutoka serikalini, vyuo vikuu, taasisi zisizo za kiserikali na sekta binafsi.

Uzinduzi huo umeenda sambamba na uteuzi wa mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa kamati hiyo ambapo Profesa Said Idd ambaye ni mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine ameteuliwa kuwa mwenyekiti na makamu mwenyekiti ni Bi Anna Maembe kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Kamati ya Kitaifa ya Ushauri ya Misitu inaundwa kwa mujibu wa Sheria ya Misitu Na 14 ya mwaka 2002 kifungu cha 10. Kazi za kamati kwa mujibu wa sheria hiyo ni kumshauri Waziri juu ya mambo yote yanayohusiana na ukodishwaji wa misitu, kutangazwa kwa hifadhi za misitu, usimamizi wa misitu ya hifadhi na mapitio ya sera ya misitu.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment