Misri yapinga mkataba wa mto Nile

Mto Nile.

Nchi saba za eneo la Afrika ya Mashariki zimetiliana sahihi mkataba utakaoziruhusu matumizi ya maji zaidi ya kile kipimo kilichozikwaza chini ya mkataba wa mwaka 1959. Hatua hii inapingwa vikali na Misri pamoja na Sudan.

Chini ya mikataba ya mwaka 1929 na 1959 asilimia 90 ya maji ya mto Nile yametengwa kwa ajili ya Misri.

Nchi zilizo katika njia ya mto huo kama Uganda, Kenya na Ethiopia yanasema hali hiyo ni dhuluma kwao na yanataka mpango mpya na kwa kipindi cha miaka kumi na mitatu ya majadiliano hakuna makubaliano yaliyofikiwa.

Nchi hizo saba sasa zinasema zitafanya mipango yao wenyewe kwenye mkutano mjini Entebbe, Uganda. Mshauri wa Sudan, Ahmed al Mufti aliyehudhuria mkutano wa Entebbe kama muangalizi amesema kuwa nchi hizi hazina sababu ya kulalama, sababu zina mvua ya kutosha.
Maji ni usalama wa taifa

Mwandishi wa BBC mjini Cairo, Wyre Davies, anasema kwa Misri, suala la maji ni suala la usalama wa taifa. Mkurugenzi wa idara ya maji nchini Kenya John Nyaro ameiambia BBC kuwa pasipo pata mfumo unaokubalika na pande zote, basi hapatokuwa na amani. Bila kuwepo utaratibu wa kisheria, hutawala sheria ya msituni ambayo haileti amani.

Ethiopia, Kenya, Tanzania, Uganda, na pia Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo, Rwanda na Burundi zimekubali kutia saini mkataba wa Entebbe, utakaowawezesha wataalamu kuamua juu ya kipimo ambacho kila nchi itaweza kutumia.

Kwa mfano Ethiopia, ambayo ina chanzo cha Blue Nile - inachangia takriban asili mia 85 ya maji ya mto Nile lakini hairuhusiwi kutumia maji yake.
Misri na Sudan hazimo

Hata hivyo Misri na Sudan zimekataa kutia saini mpango huo mpya ila tu kama utathibitisha kwamba zinapewa kiwango cha maji sawa na kile kilichopo kwa sasa.

Mwandishi wa BBC wa Afrika Mashariki, Will Ross, amesema kuwa mgawanyiko baina ya wanachama tisa wa jumuiya unaweza kuathiri juhudi za mazungumzo kuhusu jinsi ya kugawana maji hayo ikiwa nchi saba zitaafikiana peke yao.

Mshauri wa kisheria wa ujumbe wa Sudan, Ahmed al Mufti, anasema kuwa hakukuwa na sababu ya nchi hizo saba kujitenga kwa kutia saini makubaliano kwa sababu wanachama wote walikuwa wamekaribia kuafikiana.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Misri, Ahmed Abul Gheit, ameonya kuwa haki ya maji ni ''mraba mwekundu'' usiovukwa ovyo na kutishia hatua za kisheria endapo mkataba utakiukwa na nchi hizo saba.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment