DIDA FASHION YAMNYAKUA MWIMBAJI WA BONGOFLEVA Q-CHILLAH!


Na Mwandishi Wetu

MWIMBAJI wa muziki wa Bongo Fleva, Abubakar Katwila, Q-Chillah, keshokutwa Jumapili, anatarajia kufanya onyesho la utambulisho wa nyimbo zake mpya, katika Ukumbi wa Masai Club, Kinondoni, akiwa chini ya Kampuni ya Dida’s Fashion.

Aidha, shoo hilo litakwenda sambamba na kusherehekea siku yake ya kuzaliwa, onyesho linalotarajiwa kuwa la aina yake kutokana na ukimya wa muda mrefu wa msanii huyo katika muziki.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Dida’s Fashion, Hadija Seif, alisema kwamba onyesho la mwimbaji huyo litatoa picha kamili ya msanii huyo, katika kuelekea kuzindua albamu yake.

Alisema kwamba miongoni mwa nyimbo atakazotambulisha Jumapili, ni pamoja na Saba Mara Sabini, wimbo ulioanza kushika kasi katika vituo vya tedio na terevisheni hapa nchini.

“Kampuni yangu imeamua kufanya kazi na Q-Chillah kwakuwa ni msanii mzuri na mwenye uwezo wa juu katika medani ya sanaa nchini, ikiwa na lengo la kutangaza kipaji chake.

“Naamini tutafanikiwa, ukizingatia kwamba lengo ni kuhakikisha tunatangaza sanaa ya Tanzania, ndani na nje ya nchi, kitu kinachoweza kuleta maisha bora kwa wasanii wa nyumbani,” alisema.

Dida’s fashion imekuwa ikifanya kazi na wasanii mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwaandalia maonyesho ya Kimataifa, hususan nchini Uingereza, jambo linaloweza kunyanyua sanaa ya Tanzania.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment