Kikwete aitaka KCB kukiunga mkono Kilimo Kwanza!!


MWANDISHI WETU
Dar es Salaam
RAIS Jakaya Kikwete ameitaka Benki ya Biashara ya Kenya (KCB) kuchangia na kuunga mkono jitihata za serikali za Kilimo Kwanza kwa kutoa mikopo ya riba nafuu kwa wakulima hasa wa maeneo ya vijijini jambo litakalosaidia kuinua maisha yao.

Akizungumza kwa niaba ya Rais Kikwete, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano, Mohammed Seif Khatibu wakati wa hafla ya ufunguzi wa tawi la jipya la Oysterbay jijini alisema, licha ya hatua nyingi zilizochukuliwa katika kilimo biashara, uvuvi na ufugaji benki na taasisi za kifedha zina nafasi kubwa kuchangia kupunguza umaskini nchini.

Akifafanua wakati wa ufunguzi huo unaofanya idadi ya matawi yake kufikia 11 nchini alibainisha kwamba kinachohitajika kwa sasa kwa KCB na benki zingine ni kufikisha huduma zake katika maeneo walipo wananchi ili kuchangia moja kwa moja kuwawezesha wananchi kujikomboa kimaendeleo.

“Natoa changamoto kwa benki zote nchini kuchangia kubuni njia ya kuwafikia wananchi maskini moja kwa moja au kwa kupitia taasisi nyinginezo,” alisema Rais Kikwete. KCB kwa sasa imekuwa benki kubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa maana ya kuwa na zaidi ya matawi 200 na pia kuwa na rasilimali kiasi cha dola za kimarekani bilioni 2.6.

Awali Mwenyekiti wa Bodi ya KCB Tanzania Dk. Edmund Mndolwa alisema kuwa kwa sasa benki hiyo ina wanahisa 170,000/- kutoka nchi zote za Afrika Mashariki na kuweza kuajiri wafanyakazi 250 nchini wakiwemo watano kutoka nchi za nje.

Tofauti na hayo alisema licha ya kutoa huduma ya mikopo kwa wateja wadogo, wa kati na kampuni wamepanga kuboresha huduma zao kwa kutumia teknolojia ya T24 Software itakayofungwa kwenye komputa zote nchini na kuanza kutumika Juni mwaka huu.

“T24 itatusaidia kutoa kwa haraka na ufanisi zaidi, Wateja wetu sasa wanaweza kutumia huduma ya benki ya KCB katika tawi lolote lile katika nchi yoyote ile ambako tunaendesha shughuli zetu. Tayari teknolojia hii inatumika KCB Uganda, Rwanda, Sudan Kusini na Kenya kwa sasa,” alisema Dk Mdolwa.

Naye Mwenyekiti wa kundi la KCB, Peter Muthoka alisema kwamba katika kipindi cha miaka 100 walichotoa huduma benki hiyo imezidi kukua na kuendelea kuhamasisha utamaduni wa watu kuhifadhi fedha zao benki miongoni mwa wakazi wa Afrika Mashariki.

“Tunajivunia kwamba tunaendelea na safari ya kutoa huduma bora kwa wananchi ambazo zinawawezesha kuzitumiua na kufikia kwa kwa urahisi. Hili linatokana na mkakati wetu wa kufikisha huduma kwenye maeneo ya vijijini, mijini ikiwemo kunitanua zaidi katia ukanda wa Afrika Mashariki,” alisema Muthoka.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment