UBALOZI WA RWANDA KUADHIMISHA MIAKA 16!!


(Na Veronica Kazimoto – MAELEZO)
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernad Membe anatarajia kuwa mgeni rasmi katika maaadhimisho ya siku ya mauaji ya halaiki ya Kimbaari- Rwanda yatakayofanyika hapo kesho katika Kituo cha Utamaduni cha Urusi kilichopo Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo katika Ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO, Balozi wa Rwanda nchini Tanzania Bi. Fatuma Ndagiza amesema, maadhimisho hayo yanalenga katika kukumbuka na kutoa heshima kwa watu waliofariki na waliojeruhiwa kutokana na mauaji hayo.
“Katika kumbukumbu hii tutatoa heshima kwa wananchi wote waliokumbwa na mauaji haya na pia kutoa elimu kwa mataifa yote duniani ili kujua athali ya mauaji ya Rwanda na hivyo kujihadhali na mauji haya yasitokee tena katika nchi yoyote ile.” Ameongeza Bi Ndagiza.
Bi Ndagiza amebainisha kuwa, maadhimisho haya yataambatana na kutoa misaada mbalimbali kwa watoto yatima na wajane, kufanya makongamano yatakayotoa elimu kuhusu athari za mauaji ya halaiki na kutembelea makaburi ya watu waliofariki kwa ajili ya mauaji hayo.
Aidha kutokana na umuhimu wa maadhimisho hayo, Ubalozi wa Rwanda umeandaa mjadala wa wazi utakaofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam siku ya Jumamosi wiki hii, ambao utajadili masuala mbalimbali kuhusu mauaji ya kimbari ili kutoa elimu kwa baadhi ya watu wasiojua athari za mauaji haya.
Msemaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya Rwanda iliyoko Arusha (ICTR) Bwana Roland Amoussouga amesema, wiki hii mahakama hiyo itazindua mpango wa kuwahamasisha vijana juu ya umhimu wa mahakama katika kuendeleza amani kimataifa utakaofanyika Mlimani city jijini Dar es Salaam.
Bwana Amoussouga amesema mpango huu umedhaminiwa na Serikali ya Ujerumani na
utahusisha nchi za Afrika Mashariki ambazo ni Tanzania , Kenya , Uganda , Burundi na Rwanda ambapo kutakuwa na mshindano ya kuandika insha kwa wanafunzi wenye umri kati ya miaka 8 hadi 18.
Amezitaja shule za msingi zitazoshiriki katika mkoa wa Dar es Salaam kuwa ni Hazina international, St. Anne Marie Academy, Olympio, Osterbay, Bunge. Tusiime. Shule za Sekondari ni Baobab, Jangwani, Makongo, Good Samaritan, Tusiime, Mzizima, Chang’ombe na Zanaki.
Mauaji ya halaiki yalitokea mwaka 1994 katika nchi ya Rwanda eneo la Kimbari ambapo mwaka huu maadhisho hayo yatafanyika katika mkoa wa Kigali nchini Rwanda na kauli mbiu ya mwaka huu inasema,“Tukumbuke mauaji ya Kimbari huku tukidhibiti trauma – madhara ya mauaji ya halaiki.”

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment