Rais Kikwete atoa misaada ya milioni 51 kwa waathirika wa mafuriko KIlosa!!


Na Tiganya Vincent-Kilosa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Jakaya Mrisho Kikwete ametoa misaada ya jumla ya shilingi milioni 51 kwa ajili ya wakazi wa Wilaya Kilosa walioathiriwa na mafuriko.
Misaada hiyo ni kwa ajili ya kusaidia maeneo mbalimbali ya maendeleo yakiwemo elimu , ulinzi , michezo na ujenzi mpya wa makazi.

Akisoma taarifa ya Ikulu ya utoaji wa misaada hiyo juzi kwa waandishi wa habari wilayani Kilosa Waziri wa Fedha na Uchumi Mustafa Mkulo alisema kuwa Rais Kikwete aligawanya misaada hiyo imegawanyika katika taasisi mbalimbali za umma zilizomo katika wilaya hiyo.
Alitoa ufafanuzi kuwa Rais Kikwete ameagiza kuwa mipira 1,500 itolewe katika Shule zote za Msingi zilizoko katika eneo lililoathiriwa na mafuriko na pikipiki tano zipelekwe katika vituo vya Polisi vya Kimamba , Mikumi, Dumila na Polisi wilaya ili kusaidia kuimarisha ulinzi katika maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko.
Mkulo alisema kuwa redio 1,500 zitapelekwa katika shule za msingi na Sekondari katika maeneo yaliyoathiriwa ili wanafunzi hao waweze kutumia redio hizo kwa ajili ya kupata masomo waliyokosa katika maeneo ambayo hawakuyasoma kipindi cha mafuriko.
Aliongeza kuwa Rais Kikwete pia ametoa baiskeli 80 kwa ajili ya ya kuwagawia kila Ofisa Mtendaji wa Kata na Waratibu wa Elimu Kata ili waweze kusaidia shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo elimu.
Mkulo alisema kuwa kwa upande televisheni 15 zitatolewa kwa Sekondari tatu zilizoko katika maeneo yaliyoathirika na mafuriko ambapo kila moja itapata moja na nyingine mbili zitapelekwa katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi na Chuo cha Vijana wilayani humo kitapata televisheni mbili pia.
Aliongeza kuwa Chuo cha walimu kitapatiwa televisheni 4 na Chuo cha Utafiti cha Kilimo cha Ilonga (LITI) kitapatiwa televisheni mbili.
Aidha Mkulo alisema kuwa Rais Kikwete ametoa jozi 3,600 za kandambili kwa ajili ya wanafunzi wa sekondari zilizoathirika na mafuriko na kutoa mabati 554 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za baadhi ya wananchi waliothirika na mafuriko.
Vile vile Rais Kikwete ametoa vyerehani 50 kwa vikundi vya akinamama katika maeneo yaliyoathirika na Jenereta tano(5)za umeme wa upepo kwa ajili ya kusaidia kusambaza umeme katika makambi ya watu walioathirika na mafuriko hayo.
Mkulo alisema kuwa pia Rais Kikwete ametoa seti 20 za vyombo vya muziki na kuagiza vitolewe katika vyuo vilivyopo katika maeneo yaliyoathiriwa na pia ametoa mashine za maji tano kwa ajili ya vituo vya Afya vilivyoathiriwa na mafuriko.
Msaada hiyo ni sehemu ya kutimiza ahadi ya Rais Kikwete aliyowapa waathirika hao alipowatembelea mapema kwa huu.
Kiasi cha watu 23,000 bado wanaishi katika makambi ya muda katika maeneo ya Kibamba na mji wa Kilosa kufuatia mafuriko hayo.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment