RAIA WA BURUNDI WAKAMATWA RUKWA WAKIUZA SILAHA!!


Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi
Jeshi la Polisi Mkoani Rukwa limewatia nguvuni watu wawili Raia wa Burundi wakiwa na silaha moja aina ya SMG ikiwa na Risasi 127.
Kamanda wa Polisi mkoni Rukwa ACP Isunto Mantage, amesema kuwa watuhumiwa hao wamekamatwa huko kwenye kijiji cha Kabwe wilayani Nkasi wakiwa katika harakati za kutafuta sola la kuiuza silaha hiyo yenye namba NO. KI 342432.
Kamanda Mantage amewataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni Erick Niyokindi(25), na Richard Ndizeye(33), wote wakazi wa Barabara ya Saba mtaa wa Kalitye Chibitoke mjini Bujumbura Burundi ambao walikuwa wakiiuza silaha hiyo kwa bei ya shilingi milioni 2.
.
Kamanda huyo amesema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa na Makachero wa Polisi waliokuwa wakiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Mkoani Rukwa Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP. Peter Ngussa.
Amesema watuhumiwa hao walikamatwa usikuwa wa kuamkia jana wakiwa kwenye nyumba ya kulala wageni ya Duma katika kijiji hicho cha Kabwe Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa
Amesema kukamatwa kwa silaha hiyo pamoja na watuhumiwa, kunatokana na taarifa za siri kutoka kwa raia wema kuwa kuna watu wanaouza silaha ambao walikuwa katika eneo la kijiji hicho wakijifanya wafanyabiashara wa mazao wakitafuta mteja wa kumuuzia silaha hiyo.

Amesema wakati wa mahojiana na Watuhumiwa hao, walikiri kuingiza silaha hiyo hapa nchini kwa njia za panya wakitokea Bujumbura nchini Burundi tangu mwezi Oktoba mwaka jana kwa lengo la kuiuza.
Kamanda Mantage amesema ingawa bado makachero wa Polisi wanaendelea na mahojiano na watuhumiwa hao, lakini Polisi wanahisi kuwa silaha hiyo imekuwa ikitumika katika matukio mbalimbali ya kihalifu mkoani Rukwa na mikoa mingine jirani.
Katika hatua nyinge, Polisi mkoani humo pia inawashikilia watu wawili kwa tuhuma za uvunjaji wa nyumba usiku na kuiba.
Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa ACP Mantage amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Juma Ernest (37), wa Misunkumilo na Geofrey Bruno maarufu kwa jina la Makuti (37), mkazi wa Majengo mjini Mpanda mkoani Rukwa.
Kamanda huyo amesema kuwa Polisi waliendesha msako na kufanya upekuzi katika maeneo mbalimbali yaliyotajwa na watuhumiwa hao na kufanikiwa kukamata vitu mbalimbali ambavyo vilitambuliwa na wahanga waliovunjiwa nyumba zao.
Amevitaja vitu vilivyokamatwa kuwa ni pamoja na mito ya makochi, Luninga sita za aina mbalimbali, Deck tano za aina mbalimbali, Radio Cassette nne za aina mbalimbali, Magodoro mawili yenye ukubwa tofauti na baiskeli moja aina ya Sports.
Amesema tayari baadhi ya mali hizo zimetambuliwa na wenyewe na nyingine zinaendelea kutambuliwa. Watuhumiwa hao bado wanahojiwa ili kusaidie kuwapata washirika wengine wa matukio ya uvunjaji wa majumba.
Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa amewashukuru Raia wanaoendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kutoa taarifa za kihalifu na wahalifu na kuwataka wengine waige mfano huo ili kuutokomeza uhalifu nchini

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment