Twanga Pepeta 'Kupigisha Simu' Kiwalani januari 29 ijumaa!!


BENDI ya muziki wa dansi ya African Stars 'Twanga Pepeta International' inatarajia kuwapa mashabiki wake wa Kiwalani, Dar es Salaam, burudani ya staili yake mpya iliyoshika kasi ya 'Kupigisha Simu' kwenye ukumbi wa Koyanga Night Park.
Mkurugenzi wa Kampuni ya First Entertainment iliyoandaa onyesho hilo, Victorian Nachenga 'Victor Buguruni', alisema Dar es Salaam jana kuwa bendi hiyo itafanya onyesho hilo Ijumaa (Junuari 29, mwaka huu) kuanzia saa 3 usiku kwa kiingilio cha sh. 5,000.
Victorian alisema Twanga Pepeta pia itawapa mashabiki wao staili ya 'Sugua Kisigino' katika onyesho ambalo pia ni sehemu ya kuendelea kukaribisha mwaka mpya 2010 na 'kurudi nyumbani' kwenye ukumbi huo uliopo Kiwalani Kijiwe Samli.
Mkurugenzi huyo alisema onyesho hilo pia litapambwa na burudani kutoka kwa wasanii wengine watakaotangazwa baadaye.
Twanga Pepeta inayotamba na albamu ya 10 ya bendi hiyo, Mwana Dar es Salaam, itapiga nyimbo zake saba mpya zikiwamo Sumu ya Mapenzi uliotungwa na Khalid Chuma 'Chokoraa', Ubaya Aibu (Saulo John 'Ferguson'), Sitaki Tena (Saleh Kupaza), Nazi Haivunji Jiwe (Thabit Abdul).
Nyingine ni Rafiki Adui uliotungwa na Rogart Hega 'Katapila' na Shida Darasa na Mwana Dar es Salaam uliobeba jina la albamu, zilizotungwa na Charles Gabriel 'Chaz Baba'.
Albamu nyingine ambazo Twanga Pepeta imewahi kutoa na kutamba katika anga za muziki nchini ni Kisa cha Mpemba mwaka 1999, Jirani (2000), Fainali uzeeni (2001), Chuki binafsi (2002), Ukubwa jiwe (2003), Mtu pesa (2004), Safari 2005 (2005), Password (2006) na Mtaa wa Kwanza (2007).

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment