Mrisho Ngasa mchezaji wa timu ya Yanga akimiliki mpira mbele ya beki wa timu ya moro United Oscar Joshua huku Jerry Tegete akianagalia katika moja ya mchezo uliochezwa katika mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ya Vodacom.
WAKATI timu za Ligi Kuu zikiwa katika maandalizi mazito ya kuuanza mzunguko wa pili wa ligi hiyo kuanzia mwishoni mwa wiki hii, uongozi wa timu ya soka ya Moro United, unamsaka beki wake aliyesajiliwa hivi karibuni katika dirisha dogo la usajili, Abdallah Matanda.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Moro United, Eric Anthony, Matanda aliyewahi kuichezea Prisons ya Mbeya, hajaonekana mazoezini, licha ya hivi karibuni kuchukua vifaa vya timu kwa ajili ya mazoezi.
“Ni kweli, tunamtafuta kwa sababu hatujui kilichomsibu. Tangu achukue vifaa vya mazoezi hajaonekana na hata kocha, Juma Mwambusi na wasaidizi wake hawana taarifa. Mbaya zaidi ni kwamba hapatikani kupitia simu yake ya mkononi,” alisema Anthony na kuongeza kwamba; “Tunamuomba aripoti kambini haraka au popote alipo awasiliana na uongozi.”
Ukiachana na Matanda, msemaji huyo ameelezea kufurahishwa na maandalizi ya timu yake, akidai inaonyesha matumaini makubwa ya kufanya vizuri katika mzunguko wa pili.
Moro inayoshika nafasi ya tisa kati ya timu 12 kutokana na kuwa na pointi tisa, itaanza mzunguko wa pili Januari 19 kwa kucheza na Toto African ya Mwanza kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Kwa sasa timu hiyo inajifua asubuhi na jioni kwenye viwanja vya Chuo cha Ustawi wa Jamii, Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment