Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM, Asha Baraka amesema anavutiwa zaidi na mfumo wa uchaguzi utakaotumiwa ndani ya chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2010 katika kuwapata wagombea wa chama hicho.
Asha Baraka maarufu kama (Iron Lady) amesema hayo wakati alipokuwa akiongea na mwakilishi wa Tovuti ya FULLSHANGWE katika ofisi zake za ASET zilizoko Kinondoni mkabala na klabu ya Mango Garden ya jijini Dar es salaam, mwana mama huyo amesema anamshukuru mwenyekiti wa chama hicho Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Jakaya M. Kikwete.
Pia anaishukuru Kamati Kuu ya Chama hicho pamoja na Harmashauri kuu ya Chama hicho kwa kupitisha utaratibu wa wagombea wa CCM kupigiwa kura na wanachama wote wa chama hicho tofauti na utaratibu wa zamani ambapo wagombea walikuwa wakipitishwa na watu wachache hivyo kupelekea malalamiko kwa baadhi ya wagombea ambao pengine waliona hawakutendewa haki na ama kulijitokeza mianya ya rushwa.
Amesema utaratibu huu ni Mzuri na utafanya chaguzi ndani ya chama hicho kuwa ni huru na haki na kuziba mianya yoyote ya rushwa na malalamiko yasiyo ya lazima kutoka kwa wagombea watakaoshindwa katika uchaguzi ujao, Kwa mfano kuna kata 15 na kila kata ikiwa na wanachama 700 ukizidisha kwa kata hizo utapata wanachama 10500 kwa idadi hii ni vigumu mgombea kuwarubuni kwa rushwa wanachama waliowengi kiasi hiki ndiyo maana nasema uchaguzi ujao ndani ya chama chetu utakuwa huru na haki.
Asha Baraka amesema yeye anatarajia kugombea katika jimbo la Kinondoni kutokana kwa kuwa ni mkazi wa Jimbo hilo, Biashara zake anafanyia katika jimbo hilo na maisha yake kwa ujumla yamekuwa katika jimbo hilo na pia kikubwa zaidi ni kuwa amevutiwa na utaratibu wa sasa katika chama hicho kwani anaamini kwamba utakuwa ni uchaguzi safi na usio na malalamiko kutokana na mfumo wa uchaguzi uliopo ndani ya chama.
Ameongeza kwamba hata hivyo bado hajaamua agombee kupitia viti maalum, kupitia kwenye jimbo la Kinondoni au kupitia moja ya jimbo mkoani Kigoma kwa sababu hata huko ni kwake pia.
" Suala hilo bado nalifanyia kazi japokuwa wanawake wa sasa ni vyema tukajitosa kugombea kupitia kwenye majimbo ili kujipima nguvu na uwezo watu kiutendaji na kisiasa lakini pia kuleta ushindani wa kweli katika siasa za Tanzania" Anasema Asha Baraka.
0 comments:
Post a Comment