Bendera ya Taifa yaingia rasmi Kilimanjaro!!


George Kavishe Meneja wa bia ya Kilimanjaro

WANARIADHA nyota nchini, hatimaye wamefanikiwa kuifikisha bendera ya Taifa mkoani Kilimanjaro, baada ya kuikimbiza kwa siku tatu katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga.
Waliuaga mkoa wa Tanga jana mchana na kuingia Same, Kilimanjaro baada ya kupokezana bendera ya Taifa kila baada ya kilomita kati ya kumi na 12 hadi walipoingia mjini Same wakitokea Korogwe, Tanga walikopokea bendera kutoka kwa wenzao waliokimbiza kutoka Chalinze hadi Segera.
Leo wanatarajiwa kuifikisha katika mji wa Marangu, Moshi tayari kuanza kazi ya kuipandisha kileleni kabisa kwa mlima mrefu kuliko yote Afrika, Mlima Kilimanjaro kesho.
Kote walikopita, kuanzia Dar es Salaam wanariadha hao walipokelewa kwa hoihoi, nderemo na vifijo, huku waananchi wakiimwagia sifa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia Bia ya Kilimanjaro kutokana na kuasisi mbio hizo zinazotumia kaulimbiu ya “Fikisha Tanzania Katika Hatua ya Juu”.
Kufikia Same, wanariadha takribani 50 waliweza kupokezana bendera katika umbali wa zaidi ya kilomita 450 tangu walipoanza kukimbiza bendera hiyo Jumapili iliyopita katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam. Walikimbia kilomita 109 katika siku ya kwanza kati ya Dar es Salaam na Chalinze, Pwani. Siku ya pili `walizikata’ kilomita 196 kutoka Chalinze hadi Segera, Tanga kabla ya jana kuanza mbio Korogwe na kufika Same.
Meneja Masoko wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe alikuwa mwenye furaha zaidi kutokana na mbio hizo kupata mafanikio na kuvuta hisia za wengi tangu zilipoanza iku nne zilizopita.
“Nathubutu kusema nimekuwa mwenye furaha sana kwa sababu katika siku ya tatu yam bio hizi, tayari zimekuwa gumzo. Wengi wamejitokeza katika kushuhudia historia mpya ya riadha, kwani mbio hizi ni za kwanza na za aina yake.
“Kwa jinsi mwamko ulivyo, naweza kusema Bia ya Kilimanjaro itaangalia uwezekano wa kulifanya tukio hili kuwa la kila mwaka,” alisema Kavishe wakati alipokuwa anakabidhi bendera kwa mwanariadha wa kimatifa nchini, Sarah Maja aliyewaongoza wanariadha kutoka Arusha kukimbiza bendera kuanzia Korogwe.
Bia ya Kilimanjaro ndiyo inayodhamini mbio hizo zinazoshirikisha wanariadha nyota zaidi ya 70 waliobahatika kuandika historia ya kuzindia mbio hizo ndefu na za aina yake nchini.
Pia, Bia ya Kilimanjaro inawakutanisha pamoja wanariadha wa mataifa zaidi ya 25 duniani kila mwaka, kutokana na kuwa mdhamini mkuu wa mbio za kimataifa za Marathoni za Kilimanjaro `Kilimanjaro Marathon’.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment