Bobby Ricketts awapiga msasa THT!!

Hapa akizungumza na waandishi wa habari.

MSANII mahiri kutoka Marekani, Bobby Ricketts yuko nchini kuwapa
mafunzo ya jinsi ya kutumia vyombo vya muziki na kuimba, wasanii wa
kikundi cha Tanzania House of Talent (THT).
Bobby Ricketts anayeishi Denmark, ambaye ni mtaalamu wa saksafoni
katika muziki wa Soul, Funk na Jazz, alianza kutoa semina ya wiki moja
kwa wasanii hao, kwa lengo la kuwasaidia kufikia malengo yao ya kuwa
wasanii mahiri duniani.
"Lengo langu ni kuhakikisha wasanii wa THT wanatimiza ndoto yao, kwani
wana vipaji ambavyo havina budi kuendelezwa katika muziki, kucheza
dansi na maigizo," alisema Ricketts.
Rebecca Young, Meneja wa THT pia alisema: "Tunaona fahari kwa Ricketts
kujitolea kuendesha semina kwa wasanii wetu ili waweze kukomaa zaidi
katika fani."
THT imedhihirisha sanaa ni njia bora ya kufikisha ujumbe kwa jamii, na
kikundi hicho kimedhihirisha kina uwezo wa kutumia njia hiyo kufikisha
ujumbe kuhusu mada mbalimbali kwa njia ya sanaa jukwaani, ikiwa ni
pamoja na kutoa elimu ya UKIMWI.
THT wanatoa elimu hiyo kwa njia ya sanaa ikiwa ni pamoja na ujumbe
kupitia muziki, dansi na ngoma, na kimekuwa kikidhaminiwa na kampuni ya
simu za mkononi ya Zain.
Kikundi cha THT kilianzishwa mwaka 2005 na kinaundwa na vijana wapatao
45 wenye umri kati ya miaka 14 na 24. Kundi hilo la vijana limekuwa
likitoa burudani maridhawa katika matukio mbalimbali nchini.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment