UKOSEFU WA ELIMU CHANZO CHA UKIUKWAJI WA HAKI ZA WATOTO!!


Mwemnyekiti wa Tume ya haki za binadamu na Utawala Bora Jaji msitaafu Amiri Ramadhani Manento kushoto akibadilishana mwawazo na mhadhiri wa chuo cha mawasiliana ya umma na uandishi wa Habari cha chuo kikuu ca Dar es alaam Aybu Rioba katika moja ya mikutano ambayo amewahi kuhudhuria

Na Aron Msigwa na Concilia Niyibitanga – MAELEZO.
5/3/2009. Dar es salaam.
Imeelezwa kuwa kushamiri kwa vitendo vya ukiukwaji na uvunjwaji wa haki za watoto nchini kunatokana na wananchi wengi kukosa uelewa sahihi wa sheria kuhusu haki za watoto.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es salaam na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Jaji mstaafu Amiri Ramadhani Manento wakati akifungua warsha ya siku moja kuhusu haki za watoto.
Amesema kuwa hivi sasa hakuna tafsiri halisi ya nani ni mtoto kutokana na tafsiri mbalimbali za sheria kuhusu mtoto hali inayosababishwa watoto kuendelea kunyanyaswa na hivyo kuwa na haja ya kuwa na sheria moja itakayotoa tafsiri ya nani ni mtoto kwa mujibu wa sheria za nchi.
Akizungumzia kuhusu hali ya haki za watoto nchini amesema kuwa hivi sasa bado kuna utata kwa kuwa sheria za watoto zilizopo zinakinzana kwa kuwa na tafsiri mbalimbali za nani ni mtoto hivyo watu wengi wanashindwa kupata tafsiri sahihi ya mototo na haki za watoto hali inayowafanya watoto waendelee kukandamizwa na kukosa haki zao za msingi.
“Watu wengi hawaelewi kuhusu haki za watoto kwani kuna watoto ambao haki zao zinavunjwa na baadhi yao kukosa haki ya kupata elimu bora,watoto kufanyishwa kazi zaidi na pia kukosa haki ya kucheza kwa kukosa viwanja vya michezo maana maeneo mengi hayana viwanja vya michezo kutokana na ujenzi wa shule za magorofa hasa kwa shule nyingi zilizo katikati ya miji na hivyo kuwanyima haki watoto.” Amesema Jaji Manento.
Ameongeza kuwa hivi sasa kuna ulazima wa kuwa na sheria ambayo itatungwa ili kuleta usawa na kutetea haki za watoto na hivyo kuwabana wale wanaovunja haki za watoto.
Amesema kuwa kwa sasa wataalam kwa kushirikiana na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora watapeleka mapendekezo baada ya majadiliano ya warsha kwa mwanasheria mkuu wa serikali ili kuwa na sheria moja itakayotoa adhabu kwa wale watakaovunja haki za watoto .
Aidha Jaji Manento ameongeza kuwa Tume ya Haki za Binadamu itakuwa na jukumu la kutoa elimu ili kuongeza uelewa kwa wananchi waheshimu Haki za watoto.
Kwa upande wake mtoa mada katika warsha hiyo ya wadau kuhusu haki za watoto Dk. Kennedy Gastorn kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam amesema kuwa hivi sasa hapa Tanzania kuna sheria nyingi zinazohusu watoto na nyingi kuwa na kasoro,hivyo warsha hiyo ni moja ya njia ya kupatikana kwa sheria moja inayolinda haki za watoto.
Ameongeza kuwa serikali imeshakubali kuwa na sheria moja kuweza kukidhi mapungufu ya sheria za sasa kuhusu watoto na mfumo tulionao na hivyo kukidhi mikataba ya kimataifa.
Nao washiriki wa warsha hiyo wakiongea kwa nyakati tofauti wamesema kuwa hivi sasa kuna ulazima wa kuwa na sheria moja itakayotoa mwongozo na adhabu stahili kwa wale wote watakaokiuka haki za watoto.
Wameongeza kuwa mapungufu kwa upande wa elimu kwa watoto wenye ulemavu yanapaswa kuangaliwa kwa umakini kutokana na watoto wengi hasa walemavu kuendelea kubaki majumbani na wengine kukosa mahitaji muhimu katika maisha yao na hivyo kunyimwa haki zao. Wameiomba serikali kuongeza juhudi katika kuwahudumia watoto wenye ulemavu ili kuwapunguzia mzigo ili waweze kufanana na wenzao wasio na ulemavu kwa kuwawekea mazingira mazuri ya kusomea.
Pia wameiomba serikali kuweka mikakati ya kuwabana wazazi,walezi na watendaji wote wenye majukumu ya kuwalea au kutoa huduma kwa watoto watakaokiuka haki za watoto kwa kutoa adhabu kali ili haki na usawa kwa watoto viendelee kuheshimiwa.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment