MAMA SALMA KIKWETE AWAHIMIZA WALIMU KUFUNDISHA WANAFUNZI KWA BIDII!!

Mama Salma Kikwete akiwa na wanafunzi kayika moja ya shule ambazo ameshazitembelea kwa shughuli za kijamii.
Na Anna Nkinda – (aliyekuwa Iringa) Maelezo
04/02/2009 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) amewataka walimu kuwafundisha wanafunzi kwa bidii ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao ya ndani na nje ya shule.
Mama Kikwete alitoa wito huo jana wakati akiongea na walimu, wanafunzi na wananchi wa Idodi iliyopo Iringa vijijini mara baada ya kufungua nyumba ya walimu katika shule ya sekondari Idodi na kutoa vitabu kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Mwenyekiti huyo wa WAMA pia alikabidhi baiskeli kwa walemavu wanne ambao wawili ni wa kiume na wawili wa kike pamoja na kutoa kitanda cha wagonjwa ambacho kitatumika katika zahanati ya Idodi.
“Taasisi yangu ya WAMA inafanya kazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na shughuli za maendeleo hasa maendeleo ya mtoto wa kike ndiyo maana leo tumetoa msaada wa vitu mbalimbali kwa wananchi wa Idodi”, alisema.
Mama Kikwete pia aliwashauri walimu wa shule ya Sekondari Idodi kuangalia mlundikano wa wanafunzi shuleni hapo kwani kutokana na matokeo ya kidato cha nne kuwa mazuri wazazi wengi wamekuwa wakiwahamishia watoto wao shuleni hapo jambo linaloweza kusababisha kushindwa kuhimili vishindo.
Mwenyekiti huyo aliuliza, “Kwanini walimu wa shule zingine wasiige mbinu mnazotumia nyinyi kuwafundisha wanafunzi wao ili nao waweze ili kufanya vizuri katika mitihani yao kuliko kuendelea kuleta wanafunzi katika shule hii na kuleta msongamano madarasani?”
Aliwataka wanafunzi wa shule hiyo kutokufanya mapenzi wakati wako shuleni bali wakazane katika masomo kwani wazazi wao wamewajengea shule nzuri na walimu wanawafundisha vizuri hivyo kwa kutokufanya ngono watajiepusha na mimba na ugonjwa wa Ukimwi.
Nimewaletea zawadi ya vitabu naamini mtavisoma na kuvitunza naomba vitabu hivi viwe chachu ya juhudi zenu katika masomo na kuongeza kiwango chenu cha kufaulu kwani mkizingatia masomo mtafaulu zaidi na kuwa na maisha mazuri hapo baadaye”, alisema mama Kikwete.
Akisoma taarifa ya shule Mwalimu Mkuu Raimond Mlasu alisema kuwa shule hiyo ina wanafunzi 909 ambapo kati yao wa kiume ni 501 na wa kike ni 408.
Mwalimu Mlasu alisema “Shule yetu imekuwa na maendeleo mazuri kitaaluma kwani kila mwaka idadi ya wanafunzi wanaojiunga kidato cha tano imekuwa ikiongezeka hii inatokana na mahusiano mazuri yaliyopo baina ya walimu na wanafunzi”.
Kuhusiana na ujenzi wa shule mwalimu huyo alisema kuwa bado unaendelea ambapo nyumba ya mwalimu iliyofunguliwa imegharimu Tshs. 23,435,000/= mchango wa wananchi ukiwa ni Tshs. 14,435,000/= na serikali kupitia mfuko wa mpango maendeleo ya elimu ya Sekondari (MMESS) Tshs. 9,000,000/= na mbunge wa jimbo hilo alichangia mifuko 200 ya simenti.
Aliendelea kusema kuwa majengo mengine yanayoendelea kujengwa ni madarasa matatu, ambayo yapo katika hatua ya mwisho na pia shule hiyo ina mpango wa kuanzisha kidato cha tano kwa wasichana lakini wanakosa bweni la wasichana.
Kwa mwaka 2009/2010 Shule hiyo inampango wa kujenga bweni la wasichana, bwalo la chakula na nyumba ya waalimu.
Naye Mbunge wa jimbo la Isimani William Lukuvi aliwaambia wananchi na walemavu waliogaiwa baiskeli kuwa baiskeli hizo ni mali ya walemavu hao na na si mali ya kijiji
“Thamani ya baiskeli hizi ni kubwa hivyo basi mnatakiwa kuzitunza kwani zitawasaidia katika kutembelea na kuwafanya mfanye kazi zenu kwa haraka zaidi tofauti na ilivyokuwa mwanzo”, alisema Lukuvi.
Mama Salma amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani humo jana na kurejea jijini Dar es Salaam.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment