Na Mohammed Mhina na Hassan Mndeme, wa Jeshi la Polisi
Viongozi wa Vyama Mbalimbali vya Siasa vikiwemo Vyama vya Upinzani na mashirika ya ndani na yale ya Kimataifa ambayo ni Watetezi wa Haki za Binadamu, wametakiwa kuacha shutuma dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania asilindwe ama kutumia rasilimali za Serikali wakati wa kampeni za kinyang’anyiro cha Urais.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni Jijini Dar es Salaam na Mwanasheria mmoja wa Kujitegemea nchini Evod Mmanda, wakati akizungumza kwenye mkutano wa pamoja kati ya Viongozi wa Asasi za Kiraia na Jeshi la Polisi uliomafanyika kwenye Bwalo la Maafisa wa Polisi Oysterbay.
Bw. Mmanda amesema mfumo wa kisheria wa Tanzania katika maswala yanayohusu uchaguzi ni tofauti na mataifa mengine kama vile marekani ambapo hata baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu Raisi mpya hataweza kuingia madarakani hadi pale muda wa raisi aliyeko madarakani kumalizika.
Amesema hata kama baraza la mawaziri limevunjwa na wabunge wa awali kurudi katika majimbo yao kuendelea na maswala ya kampeni kwa aliyetangaza nia lakini fursa hiyo haipo kwa kiongozi wan chi kama Raisi kuiachia nafasi yake na kufanya kampeni kama mtu binafsi kwa sababu bado ana dhamana kubwa ya kitaifa.
Mwanasheria huyo amelazimika kutoa ufafanuzi kufuatia hoja iliyotolewa na Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Uchambuzi wa Sera na Maendeleo (DCDD) Bw. Chamba Kajege, kuwa, hakuna haja ya Rais anayegombea kipindi cha pili cha Urais kusindikizwa na Polisi ama kutumia rasilimali nyingine kwa kazi hiyo, na badala yake atumie rasilimali za chama.
Nae Mratibu wa kikundi cha Wanawake wenye Taaluma Bibi Zippora Shekilango, amelitaka Jeshi la Polisi kubuni mbinu zitakazowezesha kurejesha maadili mema miongoni mwa wananchi wakiwemo wanafunzi wa shule za Msingi, Sekondari na Vyuo kwani wamesema hivi sasa vijana hao na watu wazima pia maadili yao yameporomoka.
Akitoa ufafanuzi wa hoja hiyo, Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya Jinai nchini Kamishna Robert manumba amesema kuwa mmomonyoko wa maadili ni jambo linalohitaji nguvu za pamoja kati ya wazazi, walezi wakiwemo walimu na wanajamii kwa ujumla kwa vile hivi sasa kila kundi linalilaumu kundi lingine kuwa limepotoka kimaadili.
“Jeshi la Polisi linawalalamikia majambazi wanapora mgari, ukienda kwa walimu wanalaumu wazazi hawalei watoto kwa maadili mazuri, ukienda kwa wazazi nao wanalaumu walimu hawafundishi watoto vizuri, watoto nao wanasema wazazi wa siku hizi bwana, kwa hiyo tunaona kila kundi linalaumu kundi jingine” amesema Kamishna Robert Manumba
0 comments:
Post a Comment