Tasnia ya sanaa hapa nchini, inazidi kupiga hatua vijana wazidi kujimwaga katika sanaa!!


TASNIA ya sanaa hapa nchini, inazidi kupiga hatua kutokana na vijana wengi wenye vipaji na uwezo kujitokeza na kujifunza kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Sababu ya ukuaji wa haraka wa sanaa hiyo ni pamoja na kuwepo kwa utandawazi ambao ndiyo mwelekeo wa nyanja za kimaendeleo.

Rehema Ndwangira 'Loveness', ni miongoni mwa vijana chipukizi mwenye malengo ya kuifikisha mbali tasnia ya michezo ya kuigiza na sanaa kwa ujumla hapa nchini.

"Najiona naweza kuwa mwigizaji mzuri kutokana na uwezo nilionao," anasema Loveness.
Loveness anasema alijitosa rasmi katika sanaa ya maigizo mwa 2006, baada ya kujiona anaweza kuwa mwigizaji baada ya kuvutiwa na baadhi ya wasanii wengine wa ndani na nje ya nchi.
Anasema sababu nyingine iliyomsukuma kujitosa katika sanaa hiyo nu ushawishi alioupata kutoka kwa dada yake Amina ambaye naye alikuwa msanii wa kundi la Msabanzi la Magomeni, jijini Dar es Salaam.

Anasema kuwa kwa sasa yupo na kundi la Tajiquan lenye makao makuu yake Mbagala Kiburugwa, Dar es Salaam ambalo limefanikiwa kutoka na filamu ya 'Kisa Nini' iliyotungwa na Yasin Kanyama 'Kamiti'.

Loveness anasema kuwa filamu hiyo inayozungumzia mauaji ya yanayotokana na kundi la majambazi, linalosaka fedha katika filamu hiyo anaigiza kama askari mwenye lengo la kupinga vitendo hiyo.

Pia, anaigiza kama mhudumu wa hoteli ambako mwigizaji maarufu hapa nchini Charles Magali, anapigwa risasi na majambazi na kufariki dunia.
Katika filamu hiyo, Magali anaigiza kama mfanyabiashara maarufu ambaye alifikia katika hoteli hiyo, na baada ya kuawa, majambazi hao wanachukua fedha zote alizokuwa nazo, huku kundi la majambazi likiongozwa na Lamaton.

Kundi lao hilo linaundwa na wasanii 30 na limerekodi filamu yao hiyo katika Kijiji cha Mwandege.
Mbali na sanaa ya maigizo, Lovenes anasema kuwa pia kundi lao linajihusisha na michezo mingine kama karate, akiwa ni mmoja kati ya wachezaji wa mchezo huo aliyeanza kujifunza mwaka jana. Anasema kabla ya kuingia kwenye fani hiyo, alikuwa ni mchezaji wa mpira wa netiboli ambaye amewahi kuichezea timu ya Tandale Queens ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Loveness anasema akiwa na timu hiyo, amewahi kushiriki mashindano ya wilaya hiyo.
Pamoja na kupata mafanikio kidogo kupitia sanaa, malengo yake ni kuwa msanii mwenye jina kubwa katika anga za kimataifa.


Rehema Ndwangira 'Loveness' ni mtoto wa nne kwa familia ya Mzee Ndwangira ambapo kwa kupitia fani hiyo, amefanikiwa kujulikana na watu wengi, ingawa kuna ugumu ambao unajitokeza katika kazi hiyo.


Loveness anasema kwamba ugumu huo ni wasanii chipukizi kukosa nafasi kwenye vyombo vya habari kujitangaza tofauti na inavyokuwa kwa wale wenye majina makubwa.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment