Serikali inaendelea kuzichunguza halmashauri mbalimbali nchini zinazotuhumiwa kutumia vibaya fedha za Umma. Baadhi ya halmashauri zinazochunguzwa kwa sasa ni pamoja na Halmashauri ya Rombo, Ileje, Kilosa,Ngorongoro,Arusha, Mwanga na Karagwe.
Akijibu swali bungeni jana Waziri wa Nchi , Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Hawa Ghasia alisema mtumishi yeyote atakayebainika kufanya ubadhirifu wa fedha za umma atachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi, kupunguziwa madaraka na kuonywa kutegemeana na aina ya kosa.
Alisema pamoja na mambo mengine uchunguzi huo unafuatilia kwa karibu ubadhirifu kwa kukiuka sheria , kanuni na taratibu za fedha .
Aidha Waziri Ghasia alizionya Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo zimeendelea kutumia vibaya fedha za Umma kuwa kuanzia sasa mtumishi yeyote atakayebainika kufuja fedha za Umma serikali haitasita kumchukulia hatua kali. Ili kubaini kasoro mbalimbali za uendeshaji wa Halmashauri nchini, Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliagiza kufanyika kwa uchunguzi katika baadhi ya Halmashauri zilizotuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha za Umma.
0 comments:
Post a Comment