Na Lydia Churi, MAELEZO-DODOMA
Serikali imesamehewa deni la zaidi ya shilingi bilioni tano iliyokuwa ikidaiwa na nchi mbalimbali miaka mingi iliyopita.
Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Mheshimiwa Omar Yusuf Mzee aliliambia Bunge leo mjini Dodoma kuwa serikali imesamehewa deni hilo katika kipindi cha uongozi wa serikali ya awamu ya nne.
Akijibu swali la msingi la Mbunge wa Sumbawanga Mjini (CCM) Paul Kimiti ambaye alitaka kujua matumizi ya fedha hizo za msamaha iwapo zimesaidia katika maendeleo, Naibu Waziri huyo alisema fedha hizo zinalenga katika kutoa nafasi kwa bajeti ya serikali kuweza kugharamia sekta ya maendeleo.
Alisema serikali hutumia fedha za msamaha katika kusaidia miradi ya maendeleo hasa katika Nyanja zilizoanishwa ndani ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA).
Alizitaja Nyanja zilizoainishwa ndani ya MKUKUTA kuwa ni pamoja na elimu, maji, afya, kilimo, nishati na miundombinu.
Mheshimiwa Kimiti alitaka kujua ni kiasi gani serikali imesamehewa madeni ya katika awamu ya nne na fedha hizo zimetumika kwa ajili ya shughuli zipi za maendeleo ya nchi.
0 comments:
Post a Comment