JK: Nipo tayari kukosa kura zenu!!



HABARI HII NI KWA HISANI YA GAZETI LA MWANANCHI

RAIS Jakaya Kikwete jana alikutana na wazee wa MSkoa wa Dar es Salaam na kutoa hotuba kali akiwashutumu viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafabnyakazi Nchini (Tucta) kuwa ni wanafiki kwa kuendelea kushinikiza mgomo wa wafanyakazi licha ya mazungumzo yanayoendelea kati yao na Serikali.

Kwenye hotuba hiyo aliyoitoa katika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, Rais Kikwete alisema kuwa viongozi hao wa Tucta wamekuwa wakishinikiza wafanyakazi wagome kushinikiza kitu ambacho hakitekelezekiAlifafanua kuwa kima cha chini cha mshahara cha Sh315,000 kwa mwezi kinachopigiwa debe na Tucta, serikali haiwezi kukitekeleza na kama hilo ni shinikizo kwake ili wafanyakazi wampatie kura kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, hahitaji kura zao.

Rais alielezea kwa kirefu jinsi serikali ilivyotoa ushirikiano wa kukaa na kufanya mazungunzo na Tucta hadi hatua waliyofikia, lakini akasema alichoeleza Naibu Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholaus Mgaya ni kinyume na yale ambayo tayari wamekubaliana na kutiliana saini kwenye mazungumzo hayo.Kwa sababu hiyo akasema kwamba mgomo ambao ulitangazwa na Tucta uanze kesho, ni batili na mfanyakazi yoyote atakayegoma, atakuwa amevunja sheria na mwajiri ana haki ya kumchukulia hatua kulingana na kanuni zao za kazi.Rais alieleza kukerwa na msimamo wa Mgaya alioutoa katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Jumamosi ya Mei Mosi mwaka huu jijini Dar es Salaam kwamba iwapo serikali haitatangaza kima cha chini cha Sh 315,000 ndani ya siku mbili, wafanyakazi wagome.Awali kabla ya kutoa msimamo wake kuhusu mgomo wa wafanyakazi rais alirejea hotuba yake aliyoitoa mwishoni mwa Machi, mwaka huu akisema aliwasihi wafanyakazi waache mgomo na badala yake waingie kwenye mazungumzo.

Alisema Tucta waliitisha mgomo wao wakidai kwamba serikali siyo wasikivu, slakini akasema huo ni uongo ambao ulienezwa kwa makusudi na viongozi wa Tucta.“Hawa viongozi wa Tucta walisema sisi serikali ni watu wasioambilika… hawa viongozi wa Tucta ni waongo,” alisema Rais Kikwete akisisitiza kuwa hii ni moja ya sababu iliyomfanya jana awajibike kujibu.Alielezea mwenendo wa mazungumzo ya serikali na vyama vya wafanyakazi, akisema yanaendelea vizuri na kwamba baadhi ya mambo wameanza kukubalianana mengine bado wanaendelea kuyazungumza na kusisitiza kuwa imani mazungumzo yote yatafikia mahali pazuri.

Pamoja na mazungumzo hayo kufanyika, alisema kilichomkera zaidi ni kuona Mgaya kila alipokuwa anatoka kwenye majadiliano na kukutana na wafanyakazi, anazungumza tofauti na yale ambayo tayari wamekubaliana.Alisema Mgaya ni mmoja wa wajumbe waliopitisha viwango vipya vya mishahara kwa sekta binafsi na kuvitilia saini vikiwa chini ya kiwango walichokuwa wamekiwekea msimamo cha Sh315,000 kwa sekta nyingi, lakini ilimshangaza kuona anamkejeli waziri baada ya kuvitangaza.Alisema yeye Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya alivitangaza tu baada ya kupelekewa na Baraza la Mashauriano ambalo Mgaya yeye ni mmoja wa wajumbe waliovipitisha na kuvitilia saini na wala yeye kama waziri hakushiriki.“Waziri yeye hakushiriki. Alikuwa kama mtangazaji tu kwa mujibu wa sheria. Lakini cha kushangaza alimkebehi akisema viwango alivyotangaza ni danganya toto,” alieleza Rais Kikwete.Rais aliendelea kutetea hatua yake ya kuwaita viongozi wa Tucta kuwa ni wanafiki akisema hata pale walipokubaliana kwa misingi kwamba serikali haiwezi kuwalipa wafanyakazi wake kima cha chini cha Sh315,000 na wakashusha hadi wakakubaliana, bado Tucta waliendelea kugeuka walipopata fursa ya kuzungumzia hilo hadharani.

Katika kuweka sawa hilo, alisema Tucta walitoa mapendekezo yao mara tatu kwenye mazungumzo hayo na viwango vya vya mwisho serikali iliviona ni vya chini kupita kiasi ikawa imeviongeza.Viwango hivyo walikubaliana siku moja kabla ya sherehe za Mei Mosi, lakini Rais Kikwete alisema Mgaya alipokuwa anazungumza na wafanyakazi aligeuka tena na kuendelea kuwasuisitizia wafanyakazi wagome iwapo serikali haitaridhia na kutangaza kima cha chini cha Sh315,000.Rais alielezea sababu za serikali kushindwa kutekeleza kima cha chini cha Sh315,000 kwamba ni uwezo mdogo unaotokana na mapato yake.Alitoa mfano kwamba serikali ikitoa kiwango hicho itabidi iwalipe wafanyakazi zaidi ya 300,000 wa sekta ya umma Sh 6.9 trilioni kwa mwaka wakati makadirio ya makusanyo ya mapato ya serikali kwa mwaka 2010/11 ni Sh5.8 trilioni.

Akasema kwamba serikali ikilipa hivyo itabidi isimamishe shughuli zote za huduma kwa Watanzania wanaokadiriwa kufikia 40 milioni na pia ilazimike kwenda kukopa Sh 1.1 trilioni kwa wafadhili ili kukidhi haja za wafanyakazi hao zaidi ya 300,000.

Akasema yeye atakuwa mwongo kuwaahidi wafanyakazi kiwango hicho cha mshahara ambacho hakitekelezeki na hata kama ni suala la kuwafurahisha wafanyakazi hao ili wampatie kura uchaguzi mkuu ujao, hahitaji kura zao.Alisema kwamba inaelekea viongozi wa Tucta wana ajenda zao za siri ambazo alizielezea kuwa zinalenga zaidi kisiasa hivyo akawahadharisha wafanyakazi wasiingie kwenye mkondo huo.“Sasa iweje tunakubaliana hili, kesho yake asubuhi unazungumza kama hatujakubaliana,” alisema Rais na kusisitiza: “Ninayo kila sababu kuhoji dhamira zao iwapo kweli wana nia thabiti ya kuwabeba wafanyakazi ama wana lao jambo.”Alionya akisema wakiingia kwenye mkondo huo, wataathirika wenyewe na Mgaya hatakuwepo kuwasaidia.

Akamuelezea Mgaya kuwa ni mtu anayetekeleza mkakati uliowekwa na watu ambao hakuwataja na kwamba na anatekleleza hilo kulingana na alichoahidiwa.Alitishia kwamba atakayegoma atachukuliwa hatua kulingana na taratibu za kazi kwenye sekta anayofanyia kazi.Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa Tucta aliliambia gazeti hili baada ya hotuba ya Rais Kikwete kuwa hotuba yake imeonyesha ubabe na vitisho kwa wafanyakazi.

Alisema kutokana na kauli hizo kamati yao leo itajadili hotuba hiyo na kutoa tamko lake."Rais katumia lugha isiyo nzuri, hutuba yake imejaa vitisho na si demokrasia pia lugha aliyoitumia siyo nzuri na mbaya zaidi ametoa tamko lake bila ya kutusikiliza,"alisema Mgaya.Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mgomo huo ambaye pia ni Rais wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) Gratian Mukoba alimshangaa Rais Kikwete kwa kile alichosema kuwa hotuba yake imezungumzia agenda moja tu kati ya agenda tatu walizokuwa wakizijadili."Kwa muda wote tumekuwa tukijadili agenda tatu, kodi kwa wafanya kazi, maboresho ya mafao ya uzeeni na mishahara, lakini, Rais alizungumzia mishahara pekee jambo ambalo siyo haki,"alisema Mukoba na kuongeza:"Kauli ya Rais Kikwete kwamba tulikubaliana kukutana Mei 8 mwaka huu kuzungumzia suala la mishahara, siyo ya kweli kwani hata taarifa ya Baraza la Majadiliano ya pamoja inaonyesha kuwa tulikubaliana kutokubaliana," alisema.

Mapema jana asubuhi Tucta ilisema leo inatarajia kutoa tamko rasmi kuhusu mgomo wa wafanyakazi linaouandaa kufanyika nchini nzima kuanzia kesho.Mgaya aliwaambia waandishi wa habari jana ofisini kwake kuwa wanakutana kuamua mustakabali wa wafanyakazi wa Tanzania kutokana na kile walichodai kuwa serikali imeyapuuza madai yao.

Alisema kikao cha kamati tendaji kinachotarajia kukutana leo asubuhi kujadili agenda mbili, ya kwanza ikiwa ni kupandishwa kwa mishahara ya wafanyakazi wa sekta binafsi na taarifa ya maadhimisho ya siku ya wafanyakazi dunia ni (Mei mosi).“Tunakutana kujadili taarifa iliyotolewa na serikali Aprili 30 mwaka huu kuhusu kikao cha Baraza la Majadiliano kilichofanyika Aprili 27 hadi 30, pia tutatoa taarifa kuhusu mgomo wetu mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho,” alisema Mgaya.

Mvutano baina ya serikali na Tucta ulizidi kukua Jumamosi iliyopita kwenye sherehe za wafanyakazi duniani baada ya wafanyakazi kufanya sherehe mbili moja ikihudhuriwa na viongozi wa serikali.Mgawanyiko huo ulianza kujionyesha Ijumaa baada ya Chama cha Wafanyakazi Chama Cha Wafanyakazi wa Sekta ya Fedha, Viwanda, Huduma za Kibenki, Biashara (Fibuca), kutangaza kuwa kitafanyia sherehe katika Viwanja vya Mnazi Mmoja huku, viongozi wa serikali watakuwepo huku Tucta ikisisitiza kuwa sherehe zake za kitaifa zitakuwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia majadiliano yaliyofanyika hivi karibuni chini ya Baraza la Majadiliano ya pamoja alisema mazungumzo yao hayakuzaa matunda ingawa walikubaliana kuyafikisha hivyo yalivyo kwa waziri mwenye dhamana ya utumishi wa umma.Alisema katika majadiliano hayo ambayo mapendekezo yake yametakiwa kufikishwa kwa Waziri mwenye dhamana ya utumishi wa umma agenda tatu zilijadiliwa na kwamba majadiliano hayo hayakuzaa matunda.

Mgaya alifafanua kuwa suala la kodi ya mapato kwa wafanya kazi wao walipendekeza ipunguzwe kutoka asilimia 15 hadi 9, lakini serikali ikibaki na msimamo wake wa kutaka ipungue kwa asilimia mbili.Kuhusu mafao ya hitimisho la kazi, wafanyakazi walitaka serikali kuteua haraka mdhibiti na msimamizi wa hifadhi ya jamii kama sheria ya sheria ya Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Hifadhi ya jamii namba 8 ya mwaka 2008, lakini serikali ikahidi kufanya hivyo 30 Septemba mwaka huu.Kuhusu agenda ya tatu, maboresho ya mishahara alisema wao walitoa mapendekezo ya kutaka kima cha chini kiwe Sh 315,000, lakini serikali ikataka kiwa Sh 135,000 jambo ambalo hawakuafikiana nalo.

Alisema kutokana na hali hiyo, kamati ya hiyo inayotarajia kukaa leo ndio itakaoamuru mwelekeo wa uwapo wa mgomo wa wafanyakazi mara baada ya majadala huo kufanyika na kupitia taarifa hizo kwa kina.

Katika hatua nyingine, shirikisho hilo lililaani vitendo vya viongozi wa serikali kutoka katika baadhi ya wilaya nchini kuzuia wafanyakazi kushiriki sikukuu ya wafanya kazi duniani.Alitaja baadhi ya wilaya ambazo zilifanya hivyo kuwa ni wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi, baadhi ya wilaya mkoa wa Kagera kuwa viongozi wao walishiriki kudhoofisha maadhimisho hayo kwa kuzuia wafanyakazi kushiriki sherehe hizo.Alisema kundi la viongozi hao wamefanya hivyo kwa kutojua sheria na kuwa kitendo hicho na cha kusikitisha kwani kinaondoa mahusiano mazuri baina ya wafanya kazi na serikali.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment