Wanariadha mashuhuri kushiriki Kili Marathon!!


Wanariadha nguli Watanzania wanatarajiwa kushiriki kwenye mbio za Kilimanjaro Marathon ambazo zitafanyika kwa mara ya nane tarehe 28 Februari 2010. Mbio hizo zitaanza saa 12.30 asubuhi kwenye uwanja wa MUCCoBS mjini Moshi. Katibu Mkuu Msaidizi wa Riadha Tanzania, Julius Musomi alisema jana kwamba Kilimanjaro Marathon 2010 itakuwa ni onyesho la vipaji vya Tanzania katika mbio ndefu ambapo wanariadha mashuhuri kama Patrick Nyangero, Jumanne Tluway, Samwel Kwaang na Banuelia Brighton wataungana na wanariadha wengine mashuhuri.

Patrick Nyangero aliibuka mshindi wa pili kwenye mbio za km 42 mwaka jana akimaliza mbio katika muda wa 2:15:35, Jumanne Tluway alishinda pia km 42 mwaka 2008 ambapo alimaliza mbio katika muda wa 02:15:37 – akifuatiwa na Andrea Silvini (02:16:22). Samwel Kwaang ni mshindi wa km 21 mwaka jana wakati Banuelia Brighton ndiye anashikilia rekodi ya taifa kwa wanawake tangu mwaka 2008 aliposhinda km 42 katika muda wa 02:48:37 kabla ya kushinda Kigali Peace Marathon Mei 2009. Mary Naali ambaye ni kati ya wanariadha bora wa kike nchini pia atashiriki Kili Marathon.

Wanariadha wengine mashuhuri wanaotarajiwa kushiriki ni pamoja na Fabiola William, Mashaka Masumbuko, Mekiadi Bayo, Restituta Joseph, Sarah Maja, Faustine Musa, Samson Ramadhani, Damian Chopa, Ezekiel Ngimba na Sarah Kavina. Musomi amewaomba wanariadha kutoka Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Singida na sehemu nyingine za nchi kushiriki kwa wingi. “Tunapenda kumkaribisha kila mwanariadha kutoka kila mkoa nchini na nje ya nchi kuja kushiriki katika mbio hii yenye hadhi ya kimataifa.”Musomi pia amewaomba wenyeji wa Mkoa wa Kilimanjaro kujitokeza kwa wingi ili kuwapa moyo na kuwashangilia washiriki.

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, wadhamini wakuu wa mbio hizo aliwashukuru na kuwapongeza waandaaji kwa kazi nzuri kwa kuifanya Kili Marathon kuwa mbio kubwa na yenye hadhi. Kavishe alisema anaamini mbio ya mwaka huu itakuwa na ubora wa kimataifa.


Viingilio katika mbio hiyo kwa watanzania itakuwa Tsh 4,00 kwa mbio ya kilomita 42, Tsh. 3,000 kwa mbio ya kilomita 21 na sh. 2,000 kwa mbio ya kujifurahisha ya Vodacom 5km fun run. Washiriki kutoka nje ya Afrika Mashariki watalipa dola 60 kwa marathon na nusu marathon na Tsh. 2,000.Mbio hizo zimedhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, Vodacom, Tanzania Tourist Board, Tanga Cement, DT Dobie, New Africa Hotel, Goodyear Tyres, TanzaniteOne, KK Security, Keys Hotel and TPC Sugar na Kilimanjaro Water.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment