Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto inakemea vikali mauaji ya watoto wawili Mpole John (13) na Faidika John (7) wote wa familia moja, ambao walikufa papo hapo baada ya Baba yao kuwapiga kwa kitu chenye ncha kali kwa madai kuwa, mke wake aliwazaa nje ya ndoa; tukio lililotokea katika Wilaya Ngorongoro Mkoani Arusha tarehe 17 Januari, 2010 asubuhi.
Wizara imepokea taarifa ya mauji ya watoto hao kwa masikitiko makubwa maana matukio ya kikatili ya aina hii yanapotokea katika ngazi ya familia, yanarudisha nyuma kwa kiasi kikubwa juhudi za Serikali katika kuzuia na kutokomeza vitendo vya ukiukwaji wa Haki na Ustawi wa Mtoto. Aidha, mauaji haya yamewakosesha watoto haki yao ya msingi ya kuishi ambayo ni haki yao ya kikatiba na ni kitendo kinacho kinzana na Mikataba ya Kimataifa ya Haki na Ustawi wa Mtoto ambayo imeridhiwa na nchi yetu.
Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto inahimiza jamii kubadilika na kuhakikisha kuwa familia ambayo ndiyo kitovu cha wanajamii panakuwa ni mahala salama penye upendo amani na mshikamano miongoni mwa wanafamilia; na kuwapatia watoto haki zao muhimu ikiwemo haki ya kuishi, kulindwa, kutobaguliwa na kuendelezwa.
Wizara inatoa rambirambi kwa mama, ndugu na jamaa wa watoto Mpole John na Faidika John waliouwawa maana maisha yao yamekatishwa; kwani wamempokonywa haki yao ya kuishi katika umri mchanga kwa kufanyiwa ukatili wa kinyama. Wizara inawaomba wawe wavumilivu katika kipindi hiki cha majonzi mazito.
0 comments:
Post a Comment