WATOTO 246,927 KUPEWA VYANDARUA VYENYE DAWA VYA KUJIKINGA NA MARALIA MKOANI RUVUMA!!

Mama Salma Kikwete na watoto.
Na Anna Nkinda - Maelezo, Ruvuma
05/11/2009 Jumla ya watoto 246,927 walio chini ya umri wa miaka mitano wanatarajiwa kupewa bure vyandarua vyenye dawa ili kuweza kupunguza tatizo la kuugua pamoja na vifo vinavyotokana na ugonjwa wa maralia katika mkoa wa Ruvuma.
Hayo yamesemwa jana na mganga mkuu wa mkoa huo Dk. Daniel Malekela wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kugawa vyandarua bila malipo kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ulifanywa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete katika kituo cha Afya Madaba mkoani Ruvuma.
Dk. Malekela alisema kuwa walifanya sensa ya kutambua idadi ya watoto wanaostahili kupata vyandarua hivyo na jumla ya vyandarua 274,687 vimeshasambazwa katika vijiji na mitaa 539 ya mkoa huo hii inamaana kuwa kuna ziada ya vyandarua 27,760 ili na wale watoto waliozaliwa baada ya sensa kupita wapate
Licha ya kugawa vyandarua vyenye dawa mkoa huo pia unatarajia kuviwekea dawa vyandarua vipatavyo 254,400 vinavyotumika katika kaya bila jamii kuchangia gharama zozote zile.
"Tumeamua kufanya kampeni hii kwani katika tafiti ya kitaifa iliyofanywa mwaka 2007/2008 inaonyesha kuwa ni kaya nne tu kati ya 10 zinatumia chandarua kimoja chenye dawa hii inaonyesha kuwa kaya nyingi katika jamii yetu hazitumii vyandarua vyenye dawa na hivyo kuwa katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa wa malaria", alisema Dk. Malekela.
Aliendelea kusema kuwa takwimu za mwaka 2008 zinaonyesha kuwa asilimia 55 ya wagonjwa wote waliopata huduma katika vituo vya kutolea huduma wenye umri chini ya miaka mitano waliugua ugonjwa wa maralia na vifo chini ya miaka mitano vilikuwa ni asilimia 56 ya vifo vyote vilivyotolewa taarifa.
Akizindua kampeni hiyo Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa lengo la Serikali kutoa vyandarua hivi ni kuwakinga watoto dhidi ya ugonjwa wa maralia na si vinginevyo kwani kumekuwa na tabia ya baadhi ya watu kuviuza na wengine hata kuvivulia samaki haya ni matumizi mabaya ya vyandarua hivi.
Mama Kikwete alisema kuwa kila mtoto anayo haki ya kulala ndani ya chandarua kilichowekwa dawa ya kuua mbu waenezao ugonjwa wa maralia ili kupunguza kiwango cha vifo vitokanavyo na ugonjwa huo.
"Ninawaomba na ninawasisitizia wazazi wote kuwa ni muhimu kumuwahisha mtoto Hospitali pindi anapoonyesha dalili za kuugua ugonjwa wa maralia ndani ya masaa 24 hii inaweza kuokoa maisha yake kwani kumchelewesha ni hatari sana pia baadhi yenu muache tabia ya kuwapeleka watoto wenu kwa waganga wa kienyeji kwani utakuta mtoto anadalili zote za maralia lakini mzazi anampekea kwa waganga wa kienyeji jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linaweza kupelekea kifo cha mtoto wako", alisema.
Ugonjwa wa maralia unashika nafasi ya kwanza katika mkoa wa Ruvuma kwani kuna idadi kubwa ya vifo vinavyotokana na ugonjwa huo kwa kiwango cha asilimia 23.9 pia takwimu za mwaka 2004 - 2008 zinaonyesha kuna idadi kubwa ya wagonjwa wa maralia mwaka hadi mwaka. Katika kipindi hiki asilimia 50.3 ya wagonjwa wote wa maralia walikuwa ni watoto chini ya umri wa miaka mitano na zaidi ya miaka mitano walikuwa ni asilimia 49.7.
Wakati huohuo Taasisi ya WAMA iliwapatia kituo cha afya Madaba msaada wa vitanda vya kujifungulia viwili, Delivery kit moja, vitanda vya Hospitali vitano, magodoro matano, mashuka kumi,Stethosope moja, mzani wa kupimia uzito wa watoto moja, mzani wa kupimia uzito wa watu wazima mmoja na trolley dressing moja. Thamani ya vifaa vyote hivi ni Tshs.4,483,000/=.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

1 comments:

  1. Wizi Mtupu, Ufumbuzi ni kuakikisha maji yanayo tuama yanapatiwa ufumbuzi.

Post a Comment