Zaidi ya shilingi milioni mia moja kumi na mbili zimetolewa na mashirika kujenga kituo cha afya Mtimbira!!

Waziri wa Afdya na Ustawi wa Jamii Prof. David Mwakyusa.

Na Anna Nkinda - Maelezo, Ulanga
22/10/2009 Zaidi ya shilingi milioni mia moja kumi na mbili zimetolewa na mashirika yasiyo ya kiserikali ya Empower na World Lung Foundation kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Theatre, wodi ya wazazi na maabara ili kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto katika kituo cha afya Mtimbira kilichopo wilayani Ulanga katika mkoa wa Morogoro.
Hayo yamesema jana na Mkuu wa kituo hicho Dk. Eliazari Kweka wakati akisoma taarifa ya kituo kwa mke wa Rais Mama Salma Kikwete alitembelea zahanati hiyo na kutoa msaada wa vifaa mbalimbali vya afya.
Dk. Kweka alisema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa wodi ya wazazi ambayo ujenzi wake umegharimu Tshs. 45,000,000/= kutawawezesha kina mama wajawazito 16 kupata huduma ya uzazi kwa wakati mmoja.
Alizitaja changamoto zinazokikabili kituo hicho kuwa ni upungufu wa watumishi pamoja na vifaa mbalimbali vya kutolea huduma ya mama na mtoto.
Kituo hicho kinatoa huduma kwa wagonjwa wa ndani na wa nje, huduma za wajawazito na watoto, huduma za kujifungua, uzazi wa mpango, huduma za maabara,ushauri nasaha na upimaji wa Virusi vya Ukimwi (VVU) , upatikanaji wa dawa za kupunguza makali ya VVU, huduma za dharula za magonjwa ya kinywa na huduma ya kifua kikuu na ukoma.
Naye Mama Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) aliwataka wanawake wajawazito kuhudhuria kliniki na Hospitali mapema ili waweze kupata huduma na matibabu jambo mbalo litawasaidia kujifungua salama mtoto mwenye afya njema.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment