WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUANDIKA HABARI AMBAZO NI ZA KWELI!!


Na Anna Nkinda – Maelezo

13/08/2009 Serikali imewaagiza waandishi wa Habari nchini kuandika habari ambazo ni za kweli na zinazosaidia kuleta maendeleo badala ya kuandika habari ambazo zitasababisha uchonganishi na kuzidisha migogoro katika jamii.

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es salaam katika nyakati tofauti na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Joel Bendera wakati wa ziara yake ya siku mmoja ya kutembelea makao Makuu ya Klabu za Simba na Yanga ili kujionea shughuli mbalimbali za uendelezaji wa soka hapa

nchini zinafanywa na vilabu hivyo.

Naibu Waziri huyo alitoa wito huo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wanachama wa vilabu kuhusu kuwepo kwa baadhi ya waandishi wa habari ambao wamekuwa wakiandika habari zinazobabisha kutokuelewana ndani ya vilabu.

“Kwa mfano leo hii nimefanya ziara katika Klabu za Simba na Yanga lakini angalia vichwa vya habari katika baadhi ya magazeti ya kesho jinsi vitakavyoandika ni tofauti kabisa na habari yenyewe ni muhimu nyinyi waandishi wa Habari mkaangalia vichwa vya habari mnavyoviweka ili visipotoshe maana ya habari husika”, alisema.

Wanachama hao walisema kuwa ndani ya vilabu kuna watu maalum walioteuliwa kuwa ni wasemaji wa masuala yote ya klabu lakini baadhi ya waandishi wamekuwa wakimuhoji kila mtu na kuandika habari yake jambo ambalo ni la hatari ndani ya vilabu husika.

“Kuna baadhi ya waandishi wamekuwa wakitumiwa na watu fulani ili waandike habari ambazo zina maslahi kwa upande mmoja na hivyo kupotosha jamii nini kinachoendelea ndani ya vilabu”, walisema wanachama hao.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment