Victoria-falls-Zambia
Na Anna Nkinda – Maelezo 09/07/2009
Waafrika wametakiwa kutunza maporomoko ya Victoria yaliyopo katika mto Zambezi nchini Zambia ikiwa ni pamoja na kutunza mazingira ili maji yaliyopo katika mto huo yasiweze kukauka na kupoteza umaarufu wa maporomoko hayo. Wito huo umetolewa hivi karibuni na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete pamoja na Mke wa Rais wa Zambia Mama Thandiwe Banda wakati wakihojiwa na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza kutembelea maporomoko hayo yaliyopo mjini wa Livingstone. “Maporomoko haya si kwa wazambia pekee bali ni kwa waafrika na Dunia nzima kwa ujumla hivyo basi tunachotakiwa kukifanya ni kuyatunza ili yasiharibike na kuweza kutumiwa na vizazi vijavyo”, walisema. Waliendelea kusema kuwa watalii wengi wamekuwa wakifika katika maeneo hayo kuona na kujifunza mambo mbalimbali yaliyopo hapo jambo la muhimu kwa watalii hao ni kufuata masharti ikiwa ni pamoja na kutunza ya eneo husika. Naye msimamizi wa Makumbusho ya Maporomoko hayo Nobu Kunyima alisema kuwa eneo hilo linabadilika kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa kwani hadi sasa maporomoko hayo yamepitia katika sura nane. Kunyima alisema, “Kila baada ya miaka kadhaa maporomoko haya yanaonekana katika sura tofauti hivi sasa yanaonekana katika sura ya nane hii ni kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na uchafuzi wa mazingira”. Meneja Uhusiano wa Tume ya Urithi wa Taifa la Zambia Isaac Kanguya alisema kuwa maporomoko hayo ambayo ni ya kipekee hapa Duniani wanachangia kati ya nchi ya Zambia na Zimbabwe lakini kiasi kikubwa cha maporomoko hayo yanapatikana nchini Zambia. “Watu mbalimbali wanaokuja kuona maporomoko haya na kujifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na upinde wa mvua unaoonekana wakati wa usiku mara tatu kwa mwezi kuanzia saa kumi na mbili za jioni hadi saa sita usiku kati ya mwezi wa kwanza hadi wa tisa”, alisema Kanguya. Aliendelea kusema kuwa wanakabiliana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupungua kwa ujazo wa maporomoko hayo hii ni kutokana na uchafu na takataka mbalimbali zilizopo katika mto Zambezi pia kuna wakati wanakabiliana na hali ya ukame jambo ambalo linalosababisha watalii wakifika mahali hapo wanashindwa kuona maji na kuona miamba tu. Mama Kikwete aliambatana na mumewe Rais Jakaya Mrisho Kikwete aliyekuwa na ziara ya kiserikali ya siku tatu nchini humo .
0 comments:
Post a Comment