Mama Salma Kikwete.
Na Anna Nkinda - Maelezo22/07/2009 Urambo. Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amewaahidi wanafunzi wa shule ya Sekondari Kaliua iliyopo wilayani Urambo kuwapatia vitanda 22 vya mbao ili kuondokana na tatizo la kulala chini.Mama Kikwete alitoa ahadi hiyo jana mara baada ya kusikia matatizo yanayowakabili wanafunzi hao ikiwa ni pamoja na upungufu wa vitanda pamoja na mabweni jambo linalowapelekea kulala wawili wawili na wengine kulala chini.“Ninawaahidi nitawaletea vitanda mimi mwenyewe hivi karibuni tena vitanda vya mbao na si vya chuma ili muweze kuvitumia na kuepukana na tatizo mlilokuwa nalo na kulala chini au wengine wawiliwawili ila matatizo mengine mliyonayo yatatatuliwa na watu wengine kwani viongozi wote wapo hapa na wamesikia”, alisema.Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) aliwataka wazazi wafanye jitihaza za hali na mali ili kuhakikisha kuwa tatizo la mabweni linatatuliwa kwani ukasefu wa mabweni unachangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa mimba kwa wanafunzi wa kike.
Akiwa wilayani humo Mama Kikwete aliongea na wanafunzi wa kike wa shule za msingi na sekondari kutoka Kaliua pamoja na wa kata ya Urambo na kuwataka kuwa makini na maisha yao kwani wanaume anaodai kuwa wanawapenda wanawadanganya na kuwapa mimba na baada ya hapo wanawakataa jambo linalosababisha kuharibika kwa maisha yao ya baadaye.
Mama Kikwete alisema, “Kama itatokea kwa bahati mbaya umedadanganywa na kupewa ujauzito umtaje mwanaume aliyefanya hivyo ili aweze kuchukuliwa sheria na vyombo vya dola kwani wengi wenu mmekuwa mkikataa kuwataja wanaume hao kitendo kinachosababisha kuendelea kwa matukio hayo”.“Msikubali kuolewa na kukatisha masomo yenu na kama itatokea mzazi wako amekufanyia hivyo usiache kuwaambia watu ikiwa ni pamoja na kuwaeleza walimu wako ninaamini kwa kufanya hivyo tatizo hili litatatuliwa kwani jamii nzima itakuwa imesikia”. zao ili waweze kupata fedha.
Taarifa ya maendeleo ya wilaya hiyo inaonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2006 hadi Juni 2009 wanafunzi wa elimu ya msingi waliokatisha masomo yao baada ya kupata ujauzito ni 74 na wa shule za sekondari ni 40.Sababu ya wanafunzi hao kupata mimba ni hali duni ya uchumi kwa wazazi na walezi, sherehe zisizo rasmi kama vile ngoma, muziki , sinema hasa nyakazi za usiku , wanafunzi kujihusisha na vitendo vya ulevi, umbali kutoka shuleni hadi nyumbani, vitisho na unyama wanavyofanyiwa watoto wa kike hasa vya ubakaji na kulawitiwa na kuporomoka kwa maadili.
Akisoma taarifa hiyo Mkuu wa wilaya Anna Magowa alisema kuwa uongozi wa wilaya umewachukulia hatua watuhumiwa waliowapa mimba wanafunzi kwani hadi sasa watuhumiwa 17 wamefikishwa mahakamani pia matukio 52 ya mimba yamefikishwa katika ngazi za vijiji na kata ili watuhumiwa waweze kufuatiliwa na kukamatwa.“Katika kukabiliana na tatizo hili wilaya imekuwa ikikabiliana na changamoto mbalimbali kwani watoto wa kike hawawataji wanaume waliowapa mimba, ukosefu wa hosteli kwa wanafunzi wa kike, uelewa mdogo wa wazazi juu ya umuhimu wa elimu, ugumu wa kuwapata watuhumiwa kutokana na baadhi ya wazazi kutotoa ushirikiano na baadhi ya wazazi kutotoa taarifa mapewa za upatikanaji mimba kwa watoto wao”, alisema Mkuu huyo wa wilaya.
Ili kukabiliana na tatizo hilo wilaya hiyo inatoa elimu kwa jamii kwa kuwashirisha wazazi, kujenga hosteli katika shule zote za sekondari, kuwaelimisha wazazi juu ya umuhimu wa elimu, kuhakikisha kuwa walimu wa kike wanakuwepo mashuleni, kuwashirikisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuona kuwa vitendo vya rushwa vinadhibitiwa, vyombo vya sheria kutoa adhabu kali kwa watuhumiwa na kusimamia sheria ya mahudhurio namba 25 ya mwaka 1978 iliyorekebishwa kwa sheria namba 10 ya mwaka 1995 ili kukabiliana na tatizo la utoro mashuleni.Mwisho.
0 comments:
Post a Comment