Jumla ya Wanafunzi 210 wa shule za msingi na Sekondari mkoani Mwanza wameacha masomo!!

Mama Salma Kikwete
Na Anna Nkinda - Maelezo
19/07/2009 Jumla ya Wanafunzi 210 wa shule za msingi na Sekondari katika mkoa wa Mwanza wameacha masomo kutokana na tatizo la kupata ujauzito kuanzia mwezi wa kwanza hadi wa saba mwaka huu.
Hayo yamesemwa jana na Mkuu wa Mkoa huo Abas Kandoro wakati akitoa taarifa ya elimu ya mkoa huo kwa Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ambaye alitembelea Shule ya Sekondari ya wasichana ya Bwiru ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani humo.
Mkuu wa mkoa huyo alisema kuwa mkoa wake una jumla ya Shule za msingi 1213 na wasichana waliopata ujauzito ni 88 na kwa upande wa shule za sekondari zipo 267 ambapo wasichana waliopata ujauzito ni 122.
“Wilaya ya Geita ndiyo inayoongoza katika matukio ya wanafunzi kupata ujauzito na mambo yanayochangia ni pamoja na vijana kuwa na tama kwani wanarubuniwa na vitu vidogo kama simu pia wanatabia ya kuwa na wapenzi wengi na kuna wazazi wengine wanatamaa ya kupokea mahari wakati watoto wako shuleni“, alisema.
Aliendelea kusema kuwa kuna baadhi ya watendaji katika vijiji wanafanya mahakama ya kutatua tatizo hili hukohuko vijijini kwa njia ya kupokea rushwa na hivyo kukwamisha juhudi za kupambana na tatizo hili.
Kandoro alisema kuwa Serikali inafanya jitihada za kupambana na tatizo hili kwani asilimia 28 ya matukio haya yapo mahakamani, katika kata matukio yanayochunguzwa ni asilimia 17 na matukio yaliyoripotiwa Polisi ni asilimia 23.2 lakini kati ya matukio waliyoripoti asilimia 21.6 ya watuhumiwa wametoroka na asilimia 0.32 wamefungwa.
Uongozi wa mkoa huo umekubaliana kutunga sheria ndogondogo katika Halmashauri ili wasichana wanaopewa ujauzito nao wachukulie hatua hii ni katakana na tabia ya kutokuwataja waliowapa ujauzito pale kesi zinapoenda mahakamani kwani kuna wakati wanawataja lakini wakifika mahakamani wanawakana.
Naye Mama Kikwete aliwataka wanafunzi wa kike nchini kuachana na tabia ya kujihusisha na mapenzi wakiwa masomoni jambo ambalo linaweza kusababisha kupata mimba na kupoteza uelekeo wa maisha yao.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment