Mama Salma Kikwete awataka wanajamii kulisaidia Kanisa katika shughuli za maendeleo!!

Na Anna Nkinda – Maelezo
08/06/2009 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) ameitaka jamii ya Kitanzania kulisaidia kanisa katika kufanya shughuli za maendeleo ndani ya jamii.
Mama Kikwete aliyasema hayo jana wakati akihutubia katika Sherehe za kuazimisha miaka 20 ya kwaya ya Mtakatifu Kizito iliyopo Parokia ya Makuburi jimbo la Dar es Salaam.

“Nimesikia jinsi mnavyolishughulikia swala la watoto yatima na wanakwaya wasio na uwezo. Nimefurahi kwamba wameweza kupelekwa shule na kwaya. Katika kufanya hayo, watoto wa kike wamepewa kipaumbele zaidi. Haya ni mafanikio makubwa kwani wote tunaamini kuwa kumwendeleza mwanamke ni kuiendeleza jamii”, alisema mama Kikwete.
Taasisi ya WAMA ilitoa shilingi milioni mbili kwa kwaya hiyo ambazo zitatumika katika shughuli za maendeleo.
Baba Paroko wa Parokia hiyo Nico Masamba alimshukuru mama Kikwete kwa kukubali kuja kujumuika pamoja nao katika kuazimisha miaka 20 ya kwaya hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya wanafamilia Mwenyekiti wa Wanafamilia James Ngoitanile alisema kuwa wao kama walezi wa kwaya wanawashauri wanakwaya kujishughulisha na mambo mbalimbali ya maendeleo.
Msoma risala Elizabeth Mtoka alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa kwaya hiyo wamepata mafanikio mbalimbali ikiwa ni pamoja na kurekodi albamu 15 za nyimbo na Albamu mbili za video na kununua hisa katika benki ya kanisa katoliki ya MKOMBOZI zenye thamani ya shilingi laki tano.
Kwaya hiyo pia imefanikiwa kuwatia moyo wanakwaya wasio na uwezo wa kujisomesha elimu ya sekondari kujiunga na elimu hiyo muhimu kwa kuwagharimia sehemu ya ada na mahitaji madogomadogo au kwa kuwagharimia mahitaji yote muhimu na ada yote ya masomo. Kwasasa ni wanakwaya wawili tu wamefanikiwa kupata huduma hiyo kutokana na uwezo wa kwaya.

Alisema, “matatizo yanayotukabili ni uwezo mdogo wa wanakwaya wetu kiuchumi hivyo hushindwa kukabiliana na changamoto za maisha, hujuma dhidi ya kazi zetu inafanywa na wafanyabiashara wasio waaminifu kwa kurudufu kanda zetu bila idhini na kuzisambaza sehemu mbalimbali za nchi yetu na hata nje ya nchi na hivyo kuikosesha mapato kwaya. Hiki ni kilio cha awasanii wengi”.
“Ukiritimba wa usambazaji wa kanda unaomfanya msambazaji ajipangie jinsi na kiasi cha kulipa mrahaba bila kujali kabisa mabadiliko ya gharama ya maisha na ya maandalizi yenyewe”.
Kwaya hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 1988 ili kutoa huduma ya kuongoza ibada kwa nyimbo ina malengo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuanzisha mfuko wa kusomesha wanakwaya wasio na uwezo na kuanzisha mfuko wa kwaya uitwao mfuko wa mzunguko kwa ajili ya kusaidia kutoa mikopo midogo midogo isiyo na riba kwa wanakwaya.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment