MUSTAFA HASSANALI KUIKAMATA MWANZA KESHO KWA MITINDO YAKE!!

Mbunifu wa mitindo Mustafa Hassanali akiwa katika pozi na mmoja wa wanamitindo huku mwanamitindo huyo akiwa amevaa vazi lililobuniwa na mbunifu huyo.

MBUNIFU maarufu wa mavazi nchini, Mustafa Hassanali, kwa mara ya kwanza kesho (Aprili 4, 2009) anatarajia kuonyesha mitindo ya mavazi aliyobuni kwa wakazi wa Jiji la Mwanza.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Hassanali alisema onyesho hilo la mavazi alilolipa jina la 'Satolicious' litafanyika katika ukumbi wa News Mwanza Hotel kuanzia saa 2.00 usiku.
Hassanali alisema onyesho hilo pia litahusisha kazi za mbunifu wa mavazi kutoka Mwanza, Chris George na wanamitindo maarufu kutoka Dar es Salaam na Mwanza.
Onyesho hilo lililodhaminiwa na Kampuni ya simu za mkononi ya Zain Tanzania, Coca Cola na Nyanza Road Works, kiingilio kitakuwa sh. 20,000 kwa viti maalumu na sh. 10,000 kwa viti vya kawaida.
Meneja Uhusiano wa Zain Tanzania, Beatrice Mallya alisema Zain inaona fahari kudhamini maonyesho hayo na pia utakuwa ni wasaa mzuri wa kudhihirisha Ulimwengu Maridhawa wa Zain kupitia maonyesho hayo.
Hassanali alisema onyesho hilo ni mahsusi kwa wakazi wa Mwanza wanaopenda kwenda na wakati katika mavazi na watapata fursa ya kushuhudia mitindo mipya na ya kisasa inayotamba hivi sasa.
"Kama unavyojua, mambo ya Hassanali si ya kubahatisha... nawaomba mashabiki na wapenzi wa mitindo ya mavazi wa Mwanza wajitokeze kwa wingi kushuhudia mavazi yanayokwenda na wakati," alisema Hassanali.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment