MAONYESHO kabambe ya sarakasi yanayojulikana kama Zain Sarakasi Mama Afrika, yanayoendelea kuonyeshwa jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki yaliwachengua wanafunzi wa shule ya msingi Diamond na Kwanza International za Dar es Salaam. Wanafunzi wapatao 300 wa shule hizo mbili walifika kwenye viwanja vya Biafra, Kinondoni, kushuhudia maonyesho hayo ya sarakasi yaliyoonekana kuwasisimua, huku wakifaidi uhondo huo kwa muda wa saa mbili na nusu. Mmoja wa wanafunzi wa shule ya msingi ya Diamond, Samwel Shayo alisema amefurahishwa na maonyesho hayo ya sarakasi, kauli iliyoungwa mkono na mwanafunzi mwingine wa Kwanza International, Nadir Mohamed. Naye Mkurugenzi na mwandaaji wa maonyesho hayo, Winston Ruddle kutoka Zimbabwe, alisema maonesho hayo ya sarakasi yaliyodhaminiwa na Zain Tanzania yaliyoanza kurindima Biafra Januari 27, yataendelea kuoneshwa hadi Machi 8, mwaka huu, na baada ya kumalizika Dar es Salaam, yatahamia katika miji ya Mwanza na Arusha. Katika maonyesho hayo ya Biafra, tiketi zinauzwa kwa sh. 14,000 viti vyekundu, sh. 10,000 viti vya bluu na sh. 6,000 viti vya kijani na watoto walio chini ya umri wa miaka 12 wanalipa nusu ya gharama kwa viti vyekundu na bluu. Winston alisema wametoa ofa ya usiku wa akina dada kila Jumatano wanalipa nusu ya gharama kwa viti vyekundu na bluu na pia usiku wa familia kila Alhamisi watu wazima wawili waliolipa viti vyekundu na bluu, wataingia na watoto wawili wenye umri chini ya miaka 12 watakaolipiwa sh. 1,000 kila mmoja. Mkurugenzi huyo alisema shule zimepewa ofa ya kuweka oda ya kuona maonyesho hayo kwa bei maalumu ya sh. 5,000 kwa mwanafunzi na akatoa mwito kwa watu kutoa oda ya sherehe na hafla mbalimbali katika hema hilo la sarakasi. Maonyesho hayo yaliyofunguliwa Novemba 26, 2008 na Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya, pia yanaambatana na huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na chakula cha jioni, sherehe za shule, sherehe za kuzaliwa, sherehe za harusi, sherehe za kampuni, sherehe za makanisha na mikutano. Vijana 65 wanaounda kundi la Zain Sarakasi Mama Afrika, ambao wengi wao wanatoka Tanzania, wamepata mafunzo ya kutosha ya kuonesha vipaji vyao, ambavyo Watanzania wengi wanavyo. Kikundi hicho kilichoundwa mwaka 2001 kina wasanii kutoka Afrika Kusini, Kenya na Ethiopia ambao huonyesha vionjo mbalimbali na vikaragosi, mazingaombwe na mavazi zaidi ya 500 ya kitamaduni kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Sarakasi ya Zain 'yakuna' wanafunzi Dar!!
Posted by
ADMIN
You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment