





28/11/2008
MAGRETH KINABO – MAELEZO
DARAJA linalounganisha nchi ya Tanzania na Msumbiji lijulikanalo kwa jina la ‘Umoja Unity’ linatarajiwa kukamilika Septemba mwakani ili kuwezesha mawasiliano ya kibiashara na watu baina ya nchi hizo.
Hayo yalisemwa jana na Waziri Mkuu wa Msumbiji,Dk. Luisa Dias Diogo wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi wa habari ambao pia ulihudhuriwa na Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda uliofanyika kwenye hoteli ya Kilimanjaro Kempinski, Dar es Salaam.
Dk. Diogo alisema daraja hilo linagharimu dola za Marekani milioni 30 ambazo kila nchi itachangia nusu ya fedha hizo.
“Ujenzi wa daraja hilo ni kitu muhimu kwetu,kwa kuwa litawanufaisha Watanzania na Wamsumbiji pia si kwa kwa Watanzania na Wamsumbiji hata sehemu nyingine za jirani na nchi hizi,” alisema Dk. Diogo.
Dk. alisema katika mazungumzo yake na Pinda wamekubaliana kwamba kwenye daraja hilo kijengwe kituo kimoja cha ukaguzi cha mipakani ‘One Stop Border Post’ ili kurahisisha mawasiliano ya watu na bidhaa kati ya nchi hizo.
Mawaziri hao pia wamekubaliana kwamba katika kituo hicho kuwepo na huduma nyingine kama vile uhamiaji, forodha, polisi, benki, posta mawasiliano, maji,afya na umeme.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Pinda akizungumzia kuhusu umuhimu wa daraja hilo alisema litasaidia kuimarisha mahusiahano ya kibiashara kati ya nchi hizo.
“Tunaweza tukafanya biashara za aina baina ya Tanzania na Msumbiji. Inaweza kuwa ya vyakula, samaki na bidhaa nyingine kubwa kama vile nguo ndio maana tunafikiri kuwa daraja hili ni kitu muhimu. Tunahitaji kufanya biashara halali kati ya nchi hizi mbili,” alisisitiza Pinda..
Akizungumzia kuhusu ziara yake hapa nchini, Dk, Diogo alisema kwanza anawashukuru Rais Jakaya Kikwete, pamoja na Waziri Mkuu Pinda kwa kupata nafasi ya kuzungumzia zaidi masuala ya ushirikiano kati ya nchi hizo.
Dk. Diogo alisema kwa upande wa kisiasa ushirikiano ni mzuri, lakini kwenye masuala ya kiuchumi yanahitaji kuimarishwa zaidi, ambapo aliitaja miradi ambayo inahitaji kuimarishwa kuwa likiwemo daraja hilo na miradi mingine mipya ya utalii, elimu na uhamiaji.
0 comments:
Post a Comment