Hapa Bw. Richard Kasesela ambaye pia ni Afisa mtendaji mkuu wa shirika lisilokuwa la serikali (ABC Tanzania) linalojihusisha na mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi akizindua moja ya mikutano iliyowahi kufanyika hapa nchini katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
TANZANIA BASKETBALL FEDERATION (TBF)
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) ilikutana katika kikao chake cha kawaida kuzungumzia, kutolea maamuzi na kupitisha mambo kadhaa yaliyojiri wakati wa mashindano ya Taifa ya mpira wa Kikapu (Taifa Gold Cup) yaliyomalizika siku ya Jumamosi ya tarehe 1/11/2008.
Kamati ya Utendaji ilizungumzia kuhusu mambo yafuatayo:
1) Kufungiwa kwa mchezaji Mohamed Ali Dibo
2) Utovu wa nidhamu uliooneshwa na timu za mikoa ya Arusha na Shinyanga
3) Utendaji wa Kamati ya Ufundi ya TBF
4) Kikao na Mapendekezo ya Mkutano Mkuu maalum wa TBF wa tarehe 1/11/2008
5) Tathmini ya mashindano ya Taifa Gold Cup 2008
KUFUNGIWA KWA MCHEZAJI MOHAMED ALI DIBO
Kwa kawaida uendeshaji wa shughuli au mashindano yoyote ya mpira wa kikapu huwekewa taratibu au kanuni ambazo washiriki hutakiwa kuzifuata. Chama cha Mpira wa kikapu cha mkoa wa Dar-es-Salaam (DB) kama ilivyo kwa mikoa mingine wana taratibu/kanuni zao za shughuli za mpira wa kikapu. Halikadhalika Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) nalo pia lina taratibu/kanuni zake za uendeshaji wa mashindano mbalimbali katika ngazi ya taifa.
Kwa kuwa TBF ndio waratibu wa mashindano haya ya taifa, kifungu hiki cha 4.4 cha kanuni za TBF za kuendesha mashindano haya kilitumika kwa wachezaji wa mikoa (hususan DSM) kuruhusiwa kuchezea mikoa mingine kama ilivyoonekana wakati wa mashindano hayo, akiwemo mchezaji Mohamed Ali Dibo, aliyechezea Mwanza.
Kwa mujibu wa kanuni hizo, kifungu cha 4.4, mashindano ya Taifa ya mpira wa kikapu yanaruhusu wachezaji kuwa na utashi/uhuru wa kuchezea mkoa mwingine wowote wanaotaka (mbali na ule uliowasajili kwa ligi zake) mradi mkoa husika usisajili zaidi ya wachezaji watatu kutoka nje ya mkoa huo. Pia kanuni hazitoi ulazima wa kuomba ruhusa toka mkoa wanakotoka wachezaji hao.
Hivyo mchezaji kutumia uhuru huo ulioainishwa katika kifungu hiki cha Kanuni haichukuliwi kama ni utovu wa nidhamu. Hivyo Kamati ya Utendaji kwa mujibu wa Kifungu hiki cha Kanuni iliwaruhusu wachezaji zaidi ya 20 wa mkoa wa Dar-es-Salaam (si Dibo peke yake) kuchezea mikoa mbalimbali waliopenda.
Kamati kupitia kwa Katibu mtendaji itawasiliana na viongozi wa mkoa wa Dar Es Salaam. Kuangalia suala zima la huyu mchezaji Mohamed Dibo.
UTOVU WA NIDHAMU ULIOONESHWA NA TIMU ZA MIKOA YA ARUSHA NA SHINYANGA
Timu za mikoa ya Arusha na Shinyanga zilionesha utovu mkubwa wa nidhamu kwa Shinyanga kukaidi maelekezo ya barua ya TBF ya kutomchezesha mchezaji ambaye alikuwa amezuiwa kisheria. na Arusha kutumia nguvu kuzuia mchezo kati ya Mwanza na Shinyanga kwa kukaa kiwanjani, hata waliposhauriwa na maafisa wa usalama (Polisi). Vitendo hivi vilikiuka taratibu na nidhamu ya mshindano na kusababisha usumbufu mkubwa. Kamati ya utendaji imeamua kutoa barua ya onyo kali kwa timu za mikoa hii miwili baada ya mikoa husika kukiri na kuomba radhi mbele ya wajumbe wa mkutano Mkuu maalum wa TBF. Pamoja na onyo hilo mikoa imepigwa faini ya shilingi 50,000 kila moja.
UTENDAJI WA KAMATI YA UFUNDI YA TBF
Kamati ya Utendaji imegundua mapungufu kadhaa ya utendaji wa Kamati yake ya Ufundi, hata kusababisha kasoro kadhaa za kiufundi kwenye mashindano haya. Kwa hili, Kamati ya Utendaji imechukua hatua ya kutoa onyo kwa wajumbe wa kamati ya ufundi na kuangalia uwezekano wa kuiunda upya kwa mashindano yajayo. Mwenyekiti wa kamati ya ufundi anatakiwa awasilishe kati ya siku 60 muundo mpya bila kuathiri katiba.
MKUTANO MKUU MAALUM WA TBF
TBF iliitisha kikao maalum cha mkutano mkuu ambapo masuala kadhaa yalijadiliwa na kutolewa maamuzi. Pamoja na kujadili kasoro zilizopo katika kanuni za mashindano haya kwa sasa, kikao hicho kiliunda kamati ya watu watano kuangalia na kurekebisha kanuni za sasa pamoja na kutafuta mshauri mtaalam wa sheria kuiangalia upya na kupendekeza mabadiliko ya katiba ya TBF ili kukidhi mahitaji ya shughuli za mchezo wa mpira wa kikapu kwa sasa.
TATHMINI YA MASHINDANO YA TAIFA CUP 2008
Kamati ya utendaji ya TBF ilifanya kikao cha kutathmini mashindano haya na kuweka mkakati wa kuendeleza yale yote mazuri yaliyopatikana na kuyafanyia kazi mapungufu yote ili mashindano yajayo yawe ya mafanikio zaidi.
Wenu katika maaendeleo ya michezo
Richard Kasesela
Rais TBF
0 comments:
Post a Comment