Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Oliver Mhaiki (kushoto)akitangaza kwa waandishi wa habari juu ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mkutano wa 49 wa mwaka wa Umoja wa Mashauriano ya Kisheria baina ya Nchi za Asia na Afrika(AALCO) unatarajiwa kuanza tarehe 5.08.2010 hadi 8.08.2010 mjini Dar es salaam. kulia ni Mkurugenzi wa Katiba na Haki za Binadamu kutoka Ofisi ya Mwanasheria mkuu wa Serikali Mathew Mwaimu. Picha na Tiganya Vincent-MAELEZO -Dar es salaam.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya M. Kikwete anatarajiwa kufungua mkutano wa 49 wa mwaka wa Umoja wa Mashauriano ya Kisheria baina ya nchi za Asia na Afrika (AALCO) unaotarajiwa kufanyika katika hoteli ya Kilimanjaro Kempinski jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 5-8 Agosti mwaka huu (2010).
Hii ni mara ya pili kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huu. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1986 wakati mkutano kama huu ulipofanyika mjini Arusha.
Mkutano huu unatarajiwa kuhudhuriwa na wajumbe wapatao 200 kutoka ndani na nje ya nchi wakiwemo Mawaziri wa Sheria, Wanasheria Wakuu na viongozi mbalimbali waandamizi wa sekta ya sheria kutoka nchi wananchama wa AALCO na mashirika mengine ya kimataifa.
Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria na Sekretariati ya AALCO iliyopo New Delhi, India ipo katika maandalizi ya mwisho ya mkutano huu.
Katika mkutano huu, wajumbe watapokea na kujadili taarifa mbalimbali za utendaji kazi wa Umoja huu na zile zinazogusa sheria za kimataifa. Aidha, wajumbe watajadili masuala mtambuka kama mapambano dhidi ya rushwa, mabadiliko ya tabia nchi, hifadhi ya mali asili na tamaduni.
Pamoja na mambo mengine, mkutano huu utajadili changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia kwa lengo la kupata suluhu na kuzishauri Nchi Wananchama namna bora ya kupambana nazo.
AALCO, ambayo awali ilifahamika kama Kamati ya Mashauriano ya Kisheria ya Asia (ALCC), ilianzishwa mwezi Novemba 1956 baada ya Mkutano wa Bandung (Bandung Conference) wa mwaka 1955. Nchi saba waanzilishi ni Burma (sasa Myanmar), Ceylon (sasa Sri Lanka), India, Indonesia, Iraq, Japan, Misri na Syria ambazo wakati huo zilijulikana kama Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu (United Arab Republic).
AALCO, ambayo awali ilifahamika kama Kamati ya Mashauriano ya Kisheria ya Asia (ALCC), ilianzishwa mwezi Novemba 1956 baada ya Mkutano wa Bandung (Bandung Conference) wa mwaka 1955. Nchi saba waanzilishi ni Burma (sasa Myanmar), Ceylon (sasa Sri Lanka), India, Indonesia, Iraq, Japan, Misri na Syria ambazo wakati huo zilijulikana kama Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu (United Arab Republic).
Baadaye wigo ulipanuliwa na kujumuisha nchi za Afrika. Mnamo mwezi Aprili, 1958 jina la Kamati hiyo lilibadilishwa na kuwa Kamati ya Mashauriano ya Kisheria baina ya nchi za Asia na Afrika (Asian-African Legal Consultative Committee).
Mkutano wa 40 wa Kamati ya Mashauriano ya Kisheria ya Asia na Afrika uliofanyika New Delhi, India mwaka 2001 uliridhia mabadiliko ya jina na kuwa Umoja wa Mashauriano ya Kisheria baina ya Nchi za Asia na Afrika (Asian–African Legal Consultative Organisation - AALCO).
Kwa sasa AALCO ina nchi wanachama 47. Nchi hizo ni Misri, Bahrain, Bangladesh, Brunei, Botswana, Cameroon, Cyprus, Korea Kaskazini na Gambia. Nchi nyingine ni Ghana, India, Indonesia, Iraq, Iran, Japan, Jordan, Kenya, Kuwait, Lebanon na Libya.
Wanachama wengine ni Malaysia, Mauritius, Mongolia, Myanmar, Nepal, Nigeria, Oman, Pakistan, China, Qatar, Korea Kusini, Saudi Arabia, Senegal, Sierra Leone, Singapore, Somalia, Afrika Kusini, Sri Lanka, Palestina, Sudan, Syria, Thailand, Uturuki, Uganda, Umoja wa Falme za Kiarabu, Yemen na Tanzania.
0 comments:
Post a Comment