Baadhi ya washindi wa magari ya Hyundai i10 yanayotolewa na Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania kupitia promosheni yake ya ‘Shinda Mkoko’ wamesema zawadi hiyo itawasaidia kukuza uchumi wao kwani itarahisisha usafiri katika shughuli zao.
Akizungumza kwa njia ya mahojiano kutokea Dodoma baada ya kuibuka mmoja wa washindi wa promosheni hiyo, Tolino Pechaga ambaye ni fundi umeme wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) alisema anatumaini gari hilo litakamilisha ndoto yake ya kimaisha katika kujiletea maendeleo.
Akifafanua alisema, ingawa alikuwa akitumia magari ya wafanyakazi kutoka Maili mbili anakoishi hadi Udom, ujio wa Hyundai i10 utamaliza muda wa kukimbizana na basi hilo na kumpa nafasi ya kufanya kazi zake binafsi baada ya muda wa kazi kwa mwajiri wake.
“Unajua mimi ni mwajiriwa wa chuo, lakini nafanya pia kazi zangu binafsi. Usafiri ulikuwa kikwazo namba moja kufikia malengo yangu, lakini sasa kila kitu kitaenda sawa kwani tayari nitakuwa na usafiri wangu binafsi utakaorahisisha maendeleo yangu,” alisema Pechaga.
Kwa upande wake Benard Asenga wa Keko Magurumbasi jijini ambaye ni mfanyabiashara wa duka la bidhaa ndogondogo na vyakula alisema alikuwa akitumia muda mwingi na baiskeli kufuata bidhaa sokoni Kariakoo, lakini gari hilo litamuwezesha kuboresha utoaji huduma kwa wateja wake.
Aidha Asenga alifafanua kwamba mara baada ya kukabidhiwa Hundai i10 aliyojishindia atabadilisha mtindo wa biashara anaoufanya na anafikiria kuwa mjasiriamali wa kati (SME’s) na kumiliki duka la bidhaa za jumla na rejareja.
“Sasa sitatumia tena baiskeli kufuata bidhaa mjini, nafikiria kukuza biashara yangu kutoka hatua moja kwenda nyingine jambo litakaloniwezesha kukuza hali yangu kiuchumi,” alisema mfanyabiashara huyo.
Naye Simon Kihuru ambaye ni dereva wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songea alisema zawadi hiyo iliyotolewa na Vodacom Tanzania itampunguzia gharama za usafiri kwa ajili kuwapeleka na kuwarudisha watoto wake shule kwani wataweza kutumia gari hiyo kwa matumizi ya binafsi.
“Kama nilivyosoma kwenye magazeti mbalimbali kwamba gari hiyo haitumii gharama kubwa kuihudumia, kwa kuwa mimi ni dereva itaniwezesha kutunza fedha zangu baada ya kukwepa huduma za daladala ambazo sio salama sana hususani kwa watoto,” alisema Kihuru.
Akizungumza hivi karibuni kwenye hafla ya uzinduzi wa promosheni ya ‘Shinda Mkoko’ iliyopanga kuwazawadia wateja wake gari moja aina ya Hyundai i10 kila siku Mkurugenzi wa Masoko wa Vodacom Tanzania Ephraim Mafuru alisema shindano hilo litawahusisha wateja wote wa kampuni hiyo nchini na kwamba ndani ya siku 100 kila siku mtu atakuwa anajipatia gari moja.
0 comments:
Post a Comment