Banza, Jumbe kuipamba Twanga Januari 29!!

Ramadhan MasanjaBanza Stone.
WASANII nguli wa Tanzania, Ramadhan Masanja 'Banza Stone' na Fresh Jumbe anayefanya shughuli zake Marekani, wanatarajia kutia nakshi katika onyesho la bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' litakalofanyika kwenye ukumbi wa Koyanga Night Park, Kiwalani, Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Kampuni ya First Entertainment inayoandaa onyesho hilo, Victorian Nachenga 'Victor Buguruni', alisema Dar es Salaam jana kuwa Twanga Pepeta itafanya onyesho hilo Ijumaa ya Junuari 29, mwaka huu kuanzia saa 3 usiku kwa kiingilio cha sh. 5,000, huku Banza na Jumbe wakiwasindikiza.
Victorian alisema Twanga Pepeta pia itawapa mashabiki wao staili ya 'Sugua Kisigino' katika onyesho hilo ambalo pia ni sehemu ya 'kurudi nyumbani' kwenye ukumbi huo uliopo Kiwalani Kijiwe Samli.
Mkurugenzi huyo alisema onyesho hilo pia litapambwa na burudani kutoka kwa wasanii wengine watakaotangazwa baadaye.
Twanga Pepeta inayotamba na albamu ya 10 ya bendi hiyo, Mwana Dar es Salaam, itapiga nyimbo zake saba mpya zikiwamo Sumu ya Mapenzi uliotungwa na Khalid Chuma 'Chokoraa', Ubaya Aibu (Saulo John 'Ferguson'), Sitaki Tena (Saleh Kupaza), Nazi Haivunji Jiwe (Thabit Abdul).
Nyingine ni Rafiki Adui uliotungwa na Rogart Hega 'Katapila' na Shida Darasa na Mwana Dar es Salaam uliobeba jina la albamu, zilizotungwa na Charles Gabriel 'Chaz Baba'.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment