TUMIENI MASHINDANO KUJIFUZA MAADILI, SIYO KUPATA ZAWADI TU - MAMA PINDA!

Mgeni Rasmi Mama Tunu Pinda katikati akifuatilia jambo wakati wa shindano la Kisura wa Tanzania lililofanyika usiku wa kuamkia leo Movenpick Hotel kushoto ni Mwenyekiti wa SBL jaji Marck Bomnai na kulia ni meneja uhusiano wa SBL Teddy Mapunda.
MKE WA WAZIRI MKUU Mama Tunu Pinda amewataka wasichana wanaoshiriki mashindano mbalimbali ya urembo nchini watumie fursa hiyo kutambua vipaji vyao, kujifunza nidhamu na maadili mema ya kujiletea maendeleo na siyo kushindania zawadi tu.
Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wakazi wa jiji la Dar es Salaam waliohudhuria shindano la kumtafuta Kisura wa Tanzania kwa mwaka 2009 lililofanyika jana usiku (Alhamisi, Desemba 17, 2009) kwenye hoteli ya Movenpick jijini Dar es Salaam.
“... Natoa wito kwa wasichana wetu walioshiriki mashindano haya na wengineo nchini watumie fursa hizi kwa kujifunza nidhamu na maadili mema ya kujiletea maendeleo... mashindano haya yasiwe ya kupata zawadi tu bali yawe ya kujenga misingi ya kujitambua vipaji walivyonavyo,” alisema.
Amewasisitizia kwamba pamoja na lengo la kuwa Kisura wa Tanzania, tegemeo lao kubwa liwe ni kupata elimu zaidi ya kujinasua katika umaskini na kujilete amaisha bora. “Jambo lolote likifanywa kwa nidhamu ni rahisi kufanikiwa,” alisema.
Alisema kama nchi, Tanzania inakabiliawa na changamoto ya kukuza sanaa ya kuitangaza jamii yake kama Watanzania kupitia mashindano kama hayo ya kumsaka Kisura wa Tanzania kwa kuwajengea vijana uwezo ili waipende nchi yao, wapende bidhaa zao na utamaduni wao.
Mama Tunu Pina alikabidhi hundi ya sh. milioni tano kwa mshindi wa shindano hilo, Diana Ibrahim kutoka Mara ambaye pia amepata mkataba wa kufaya kazi za Serengeti Breweriers kwa mkataba wa mwaka mzima kama balozi wa kampuni hiyo. Nafasi ya pili imechukuliwa na Jacqueline Benson wa Mwanza na ya tatu imenyakuliwa na Mwajabu Juma wa Arusha.
Mapema akizungumza na washiriki na watazamaji wa onyesho hilo, Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano ya jamii wa Serengeti Breweries, Bi. Teddy Mapunda alisema chini ya mkataba huo, Kisura huyo atapaswa kufanya kazi za kijamii ikiwemo ya kutembelea kituo cha watoto yatima cha Udesa kilichopo tarafa ya Mpimbwe, wilayani Mpanda, Rukwa.
Alisema kituo hicho kitapatiwa hundi ya sh. milioni mbili za kukisaidia kijiendeshe na pia kitapatiwa kreti 20 za kinywaji aina ya VITAMALT kama mtaji ili fedha zinazotokana na mauzo zitumike kuendesha mradi huo. Pia aliahidi kukipatia kituo hicho vifaa vya kupozea.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment