Wanawake wanaopigwa na kuachwa na waume zao wilayani Mbarari kwa kupima virusi vya ukimwi watakiwa kutoa taarifa kwa Mama Kikwete

Mama Salma Kikwete.
Na Anna Nkinda - Maelezo, Mbarali
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amewataka wanawake wilayani Mbarali ambao watapigwa na waume zao au kupewa talaka kutokana na kitendo cha kwenda kupima virusi vya Ugonjwa wa UKIMWI wampe taarifa ili aweze kuchukua hatua na kulishughulikia tatizo hilo.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alitoa wito huo jana wakati akiongea na wananchi wa wilaya hiyo mara baada ya kukabidhi msaada wa vifaa mbalimbali vya afya katika Hospitali ya wilaya Mbarali.
Aidha Mama Kikwete alitoa namba yake ya simu ya mkononi ambayo ni 0754294450 kwa wanawake hao ili waweze kumpigia au kumtumia ujumbe mfupi wa maneno pindi waume zao watakapowanyanyasa kutokana na kitendo cha wao kwenda kupima kwaajili ya kujua afya zao.
"Baadhi ya wanaume siyo waaminifu katika ndoa zao wanakuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanawake wengine na hivyo kuhatarisha usalama wa ndoa zao kwani wengi wao ndiyowanaoleta UKIMWI majumbani, sasa kwanini wewe uwe na ujasiri wa kwenda kupima yeye aje kukupiga au kukupa talaka? Huu si unyanyasaji wa kijinsia?", aliuliza Mama Kikwete.
Aliendelea kusema kuwa ili kupunguza kasi ya maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI katika wilaya ya Mbarali kila mtu anatakiwa kuwa mwaminifu kwa mpenzi mmoja aliyekuwa naye au kama hatakuwa mwaminifu achukue tahadhari.
Akisoma taarifa ya huduma ya afya na uzazi Dk. Somoka Mwakapalala ambaye ni mganga mkuu wa wilaya ya Mbarali alisema kuwa wilaya hiyo ina jumla ya wanawake wenye uwezo wa kuzaa (kuanzia miaka 15 - 49) 69,420.
Alisema kuwa idadi ya akina mama wanaojitokeza katika upimaji wa VVU kwa hiari ili kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT) ni ndogo kwani kwa mwaka 2008 wanawake wajawazito waliohudhuria kliniki walikuwa 11,875 na waliokubali kupima kwa hiari walikuwa 4583 sawa na asilimia 39".
Dk. Somoka alisema, "Hali hii inatokana na baadhi ya kina baba kuwazuia wake zao wasipime na kama wakipima kwa siri na kugundulika kuwa wameammbukizwa virusi vya UKIMWI wanawake hao hutalikiwa kwa lazima na waume zao pia ushiriki mdogo wa kina baba katika kuboresha Afya ya uzazi na upimaji wa Virusi Vya UKIMWI (VVU)".
Hospitali hiyo imepata mashine mpya ya kupima Virusi vya Ukimwi (CD4 Machine) kutoka shirika lisilo la kiserikali la Walter Reed na hivyo kupunguza kero kwa akinamama ya kusubiri majibu ya vipimo kwa muda mrefu.
Aliendelea kusema kuwa, Katika kampeni ya upimaji ya hiari ya mwaka 2007 watu waliojitokeza kupima kwa hiari walikuwa ni 24, 350 kati ya hao wanawake ni 14,875 na wanaume ni 9,475 waliopatikana na virusi vya UKIMWI ni 3,186 sawa na asilimia 13.1.
"Idadi ya watu waishio na virusi vya UKIMWI waliosajiliwa katika vituo vya kutolea dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo ni 5,410 kati ya hao wanaotumia dawa ni 2118 sawa na asilimia 39.2", alisema.
Wilaya hiyo ina vituo 47 vya kutolea huduma ya afya kati ya hivyo vinavyotoa huduma za Afya ya uzazi na mtoto ni 34 na vinavyotoa huduma ya kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ni 12.
Ili kuboresha huduma ya uzazi katika Hospitali hiyo, Taasisi ya WAMA ilitoa vitanda vya kujifungulia viwili, Delivery kit moja, vitanda vya Hospitali vitano, magodoro matano, mashuka kumi,Stethosope moja, mzani wa kupimia uzito wa watoto moja na mzani wa kupimia uzito wa watu wazima mmoja . Thamani ya vifaa vyote hivi ni Tshs.5,783,000/=

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

1 comments:

  1. HONGERA MAMA...NNA IMANI UTAISHUGHULIKIA HILO....

Post a Comment